Celina Mathew
Freeman Mbowe |
MAHAKAMA Kuu imetoa zuio la muda
kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, hadi shauri lake la msingi
katika kesi ya Kikatiba litakaposikilizwa keshokutwa Februari 23.
Februari 10 mwaka huu, Mbowe alifungua kesi ya
kikatiba dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam, Paul Makonda; Kamanda wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa
Kanda hiyo, Kamilius Wambura.
Akizungumza Dar es Salaam jana nje ya Mahakama
Kuu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema hatua hiyo imetokana na uamuzi
uliotolewa na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo, kuhusu agizo la Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda.
Alisema mahakama hiyo imeamua wanaotaka
kumkamata Mbowe, wazuiliwe hadi shauri la msingi alilofungua litakaposikilizwa.
“Hivyo Mahakama imetoa zuio la muda hadi
kesi itakaposikilizwa siku ya Ijumaa saa 7:30 mchana, ikiwa na maana kuwa
polisi wamezuiliwa kumkamata Mbowe na Mahakama imesema watakuwa na uwezo wa
kumwita kwa mahojiano, kama watataka na si kumkamata,” alisema Lissu akinukuu
uamuzi wa majaji hao.
Aliongeza: “Kwa maana hiyo mbinde za
kina Sirro zimezuiliwa kwa muda mpaka siku hiyo ya Ijumaa maombi yenyewe
yatakaposikilizwa.”
Lissu alisema kuwa Mahakama hiyo pia imetoa
ruhusa kwa mleta maombi (Mbowe), kurekebisha maombi aliyopeleka mahakamani, ili
kumjumuisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kwenye mashauri hayo na kufanya
marekebisho mengine madogo yanayofaa kwenye shauri hilo.
Mahakama imeamua marekebisho yafanywe
hadi kufikia Februari 27 mwaka huu na yatajibiwa baada ya Machi 6, ndipo watakutana
tena mahakamani hapo Machi 8 mwaka huu saa 8:00 mchana,” alisema Mwanasheria
huyo.
Lissu aliongeza kuwa ugomvi wa zuio hilo,
unaendelea Ijumaa mchana na Mahakama
itakuwa ya wazi na si kama ilivyokuwa jana ambapo ilisikilizwa chemba ambako
waandishi walizuiliwa kuingia.
Mbowe aliingia mahakamani hapo saa 10:18,
akiambatana na baadhi ya viongozi wa Chadema wakiwemo waliotangulia kabla yake,
akiwemo Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji na Naibu Katibu Mkuu Bara, John
Mnyika.
WEngine ni Lissu, Naibu Katibu Mkuu
Zanzibar, Salum Mwalimu na wengine na aliondoka 13:14 akiwa na gari yake
iliyokuwa imeandikwa KUB ikimaanisha Kiongozi wa Upinzani Bungeni, aina ya Land
Cruiser.
Kesi ya Mbowe dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salam, Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi
wa Kanda hiyo, ilisajiliwa kwa jina la Kesi ya Kikatiba namba 1 ya 2017 kwenye Mahakama ya Kuu masijala ya Katiba
(Masijala Mkuu).
Kwenye Kesi hiyo, Mbowe aliomba Mahakama Kuu
itamke na kuwa Mkuu wa Mkoa hana mmalaka ya kudhalilisha na kukamata.
Mbowe pia aliiomba Mahakama itengue vifungu vya 5&7 vya Sheria ya Tawala za Mitaa, kwakuwa ni batili na vinakiuka haki za kikatiba.
Katika kesi hizo Mbowe aliwakilishwa na mawakili
toka Kurugenzi ya Katiba Sheria na Haki za Binadamu ya Chadema.
0 comments:
Post a Comment