Jemah Makamba
MKAZI wa Sitakishari Dar es Salaam,
Christina Thomas (28), amekataa kudhaminiwa ili arudi rumande na msichana wake
wa kazi ambaye alishindwa masharti ya dhamana.
Christina jana alifikishwa Mahakama ya
Wilaya ya Ilala kwa tuhuma za kumpiga mtoto wake wa miaka miwili na
kumsababishia majeraha makubwa, kuzimia na kushindwa kumpeleka hospitalini.
Mwendesha Mashitaka Hilda Kato, alidai
mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ritha Tarimo kwamba mshitakiwa siku
isiyofahamika Januari, alimpiga kwa fimbo mtoto huyo na kumsababishia majeraha.
Kato alidai katika mashitaka ya pili,
mshitakiwa huyo ambaye ni mama mzazi wa mtoto huyo na msichana wake wa kazi,
Blanka Benjamin kwa uzembe walimwacha mtoto huyo bila kumpeleka hospitali huku
akiwa na hali mbaya ambayo ilisababishwa na mama mzazi.
Baada ya kusomewa mashitaka, mama huyo alijibu
kuwa hakumbuki, huku mshitakiwa wa pili ambaye ni msichana wa kazi akikana mashitaka
yake.
Mwendesha Mashitaka alimwambia Hakimu
Tarimo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, lakini dhamana yao iko
wazi kama watakidhi masharti.
Hakimu alitoa masharti ya dhamana kwa
washitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika mmoja akiwa mtumishi kwenye
taasisi inayofahamika na kusaini dhamana ya Sh 800,000 kila mmoja.
Baada ya kusomewa masharti hayo ya
dhamana mshitakiwa namba moja alikidhi masharti ya dhamana huku wa pili
akishindwa kutokana na wadhamini kuchelewa.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo wa kwanza
ambaye ni mama wa mtoto alisema hawezi kuwa nje kwa dhamana akimwacha mshitakiwa
wa pili rumande hivyo kumwomba hakimu warudi wote ndani hadi kesho
watakapotimiza masharti ya dhamana pamoja.
Hakimu alimwambia mshitakiwa huyo kwamba
kwa sababu yeye ana mtoto mdogo hivyo angeweza kutoka na kumwacha mshitakiwa wa
pili na kesho (leo) angepata dhamana, lakini akasema mtoto wake ataondoka na
baba yake, na yeye atarudi rumande hadi watakapopata dhamana wote wawili.
0 comments:
Post a Comment