Mwandishi Wetu
Khamis Mgeja |
WABUNGE wameshauriwa kuzidi kunoa meno
ya Bunge kama lilivyokuwa Bunge la Tisa na kuepuka kuwa tawi la Serikali kwa
kuhakikisha inaisimamia Serikali, kuishauri na kuipa maelekezo kwa mujibu wa
Katiba.
Ushauri huo ulitolewa jana na Mwenyekiti
wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja.
Alisema kuwa anatambua mara kadhaa
imetokea wabunge kusimamia maslahi ya vyama katika shughuli za kibunge, jambo ambalo
limekuwa halina tija kwa taifa na kuwakumbusha wabunge kuwa wao ni wawakilishi
wa wananchi waliowachagua na si vyama.
Ili kuhakikisha wanasimamia misingi yao
ya kibunge, wanapaswa kuwa na kuli mbiu ya kutanguliza Tanzania kwanza na
kuyaweka kando maslahi ya vyama vyao. Wanapaswa pia kuona umuhimu wa kujadili
mambo makubwa yanayolitafuna taifa kwa uwazi kama ambavyo wamediriki
kuzungumzia ukame na njaa inayoelekea kulikumba taifa.
“Hapa tulipofikia kwa mwenendo wa
Serikali yetu Bunge halina budi kunoa meno. Lisimamie misingi yake ambayo ni
kuwakilisha umma uliowachagua na si kuangalia matakwa ya vyama vyao ama kuwa
wakala au tawi la serikali, bali lisimame kwa mujibu wa Katiba,”alisema Mgeja.
Alisisitiza kuwa Bunge halipaswi
kuitetea Serikali katika kukandamiza demokrasia kwa kukomoa vyama vya upinzani
kutofanya mikutano,pia kuvifunga midomo vyombo vya habari kwa kuvitungia sheria
kandamizi hatua ambayo itachochea usiri na ubadhiru,na ukiukwaji wa utoaji haki
kwa umma.
Aidha aliwaomba wabunge hao kutoa
msimamo wa pamoja juu ya hatima ya Katiba mpya kwa sababu mchakato wake
umetumia mabilioni ya fedha za Watanzania.
Mgeja ambaye mbali ya kuongoza taasisi
hiyo, pia ni Kada maarufu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), aliwakumbusha
wabunge hao kuhoji Serikali sababu iliyofanya baadhi ya nchi kusitisha misaada
ya ufadhili kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar,kama vile MCC la
nchini Marekani,ambapo ufadhili wa fedha hizo zilikuwa muhimu kwa ustawi wa
Taifa.
Alikumbusha Bunge hilo litambue kwamba
umaskini wa Watanzania na nchi kwa ujumla unasababishwa na kutosimamia
vizuri rasilimali za nchi,na kuwaomba
kuhakikisha wanapitia upya kwa uwazi mikataba ya wawekezaji ambao kipindi hiki
wanavuna rasilimali.
“Nawaomba wapitie upya na kwa uwazi
mikataba ya Madini,Gesi,mafuta na makaa ya mawe,mashamba,viwanda zikiwemo na
rasilimali zingine;ikiwemo Nishati ya Umeme;kuona kama ina manufaa ya
Nchi,pindi Bunge likibaini haina liweke azimio la kuifuta,”alisema Mgeja.
Pia aliwaasihi katika kuhakikisha
rasilimali za nchi zinanufaisha wananchi kabla ya mikataba mipya kufungwa,ni
budi wakajifunza katika baadhi ya Nchi ambazo zinanufaika na rasilimali
zao,zimetumia mbinu gani kufanikisha hilo.
Katika kuhakikisha Bunge linatekeleza na
kusimamia majukumu yake ni vyema likahoji
kuhusiana na ununuzi wa ndege mbili zilizonunuliwa na serikali je sheria
za manunuzi zilifuatwa pia mkataba kati ya serikali na ATCL kuwa wazi kwakuwa hizo fedha ni za
umma walipa kodi hivyo wangependa kujua kupitia bunge.
0 comments:
Post a Comment