Mwandishi Wetu, Tabora
MKE wa Rais, Mama Janeth Magufuli na Mke
wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa wametoa mwito kwa Watanzania kujenga
utamaduni wa kutembelea vituo vya wazee na watu wenye mahitaji maalumu na kutoa
misaada ili kujikimu.
Walisema hayo jana walipotembelea makazi
ya wazee wasiojiweza na walemavu watokanao na ukoma ya Amani Ipuli mjini hapa.
Katika makazi hayo walikabidhi tani 7.5
za vyakula ukiwamo mchele, unga wa sembe na maharage; pamoja na mafuta maalumu ya
kujipaka watoto wenye ulemavu wa ngozi wanaosoma shule mbalimbali mkoani hapa.
Mama Magufuli alipongeza watumishi
wanaofanya kazi kwenye makazi ya wazee na watu wenye mahitaji maalumu kwa
sababu kazi hiyo ni ngumu na yenye changamoto nyingi.
“Ibada si kwenda nyumba za ibada pekee
bali hata kutembelea wazee, watu wenye mahitaji maalumu na wasiojiweza, utakuwa
umetoa sadaka kubwa kwa Mwenyezi Mungu.
Nawaomba tujitahidi kuwatembelea,” alisema.
Mama Majaliwa aliomba wananchi wawe na
utaratibu wa kusaidia wazee wanaoishi kwenye makazi hayo, walemavu na
wasiojiweza nchini na kuwafariji kwa sababu wanahitaji upendo na faraja zao.
Mwenyekiti wa Wazee waishio katika makazi
hayo, George Busambilo aliwashukuru wake hao wa viongozi kwa niaba ya wenzake
na kuwaomba waendelee na moyo huo wa kusaidia watu wasiojiweza na wenye
mahitaji maalumu.
0 comments:
Post a Comment