Seif Mangwangi, Arusha
Onesmo ole Nangole |
MAHAKAMA ya Rufaa imetupilia mbali
rufaa iliyokatwa na Chadema kupinga kutenguliwa ubunge kwa mbunge wa Longido,
Onesmo ole Nangole.
Hatua hiyo imetokana na kukiuka amri ya
Mahakama iliyowataka kufanya marekebisho kwenye maeneo mawili ya rufaa
yao na badala yake mawakili wakafanya marekebisho sehemu kubwa ya
rufaa.
Akisoma uamuzi wa jopo la majaji watatu,
Bernad Luanda, Mussa Kimpeka na Stela Mgasha, Msajili wa Mahakama hiyo, Amir Msumi
alisema Mahakama imeondoa rufaa hiyo kutokana na kukiukwa kwa amri yake.
Alisema warufani waliamriwa kufanya
marekebisho kwa kuongeza wadaiwa wawili ambao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali
na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Longido, lakini badala yake
rufaa imefanyiwa marekebisho na kuongeza mambo ambayo hawakuamriwa, hivyo Mahakama
inaiondoa rufaa hiyo.
Wakati wa kuanza kusikilizwa kesi hiyo
Februari 20, Wakili Dk Masumbuko Lamwai, aliyekuwa akimtetea mgombea wa CCM, Dk Steven
Kiruswa aliwasilisha pingamizi mahakamani kuiomba Mahakama hiyo kuitupilia
mbali rufaa hiyo iliyokatwa na mgombea wa Chadema, kwa kuwa ilikiuka amri na
maelekezo yake ya kufanya marekebisho kwa kuongeza wadaiwa wawili tu.
Aidha, Mahakama hiyo iliwaamuru wakata
rufaa kulipa gharama za kesi za wakili mmoja badala ya watatu, ambao ni Dk
Lamwai, Edmund Ngemela na Daud Haraka.
Baada ya uamuzi huo, aliyekuwa mgombea
ubunge kupitia CCM, Steven Kiruswa, aliipongeza Mahakama kwa kutenda haki
kutokana na kasoro zilizojitokeza wakati wa uchaguzi mkuu Oktoba mwaka juzi.
Alisema Mahakama imetenda haki
hivyo kupata matumaini ya mfumo wa haki kutupilia mbali rufaa hiyo na hiyo
inathibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu ulikuwa sahihi na kusisitiza kuwa
ukweli umebainika na ndiyo maana haki imepatikana.
Dk Lamwai alisema hukumu imejikita
kwenye marekebisho, hivyo anaomba upande ulioshindwa kukubali matokeo na
kuwezesha uchaguzi kurudiwa ili wananchi wa Longido wapate mwakilishi.
Alisema kesi hiyo imechelewesha muda na
kuwanyima haki ya maendeleo wananchi wa Longido na haiwezekani kukaa bila
mbunge.
Wakili Method Kimomogolo aliyekuwa
akimtetea Nangole, alisema wanatafakari uamuzi huo na kuangalia usahihi
wake, ili wasonge mbele na kudai kuwa rufaa haijatupwa, kwa sababu
haikusikilizwa na bado ipo nafasi ya wao kusikilizwa hivyo wataendelea
kuwasiliana na mteja wao ili kuona kama watakata rufaa nyingine.
0 comments:
Post a Comment