Salha Mohamed
Askofu Gwajima na Yusuf Manji |
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima, Josephat Gwajima amemtembelea Mshauri wa Kampuni ya Quality Group,
Yusuph Manji aliyelazwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Manji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya
Mbagala Kuu, alifikishwa kwenye taasisi hiyo Febuari 12 akitoka Polisi kutokana
na maradhi yanayomsumbua.
Manji alifika Kituo Kikuu cha Polisi
Febuari 9 kuitika agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kile
kinachodaiwa kuhusika na dawa za kulevya.
Akizungumza na Gazeti hili jana Dar es
Salaam, baada ya kumjulia hali Manji, Gwajima alisema alimwombea na anaendelea
vizuri.
“Nimetoka kumwangalia na kumjulia hali
Manji, nimemwombea sala fupi, lakini anaendelea vizuri,” alisema Gwajima.
Gwajima ni miongoni mwa watu waliotajwa
na Makonda akidaiwa kujihusisha na dawa za kulevya na alishikiliwa na Polisi na
ndiko walikutana na Manji.
Gwajima alitoka Polisi Febuari 11 huku
Manji akiendelea kushikiliwa hadi alipopata maradhi ghafla na kupelekwa
hospitali.
Februari 12, Gwajima alikaririwa na
gazeti hili akisema hadi alipoachwa kutoka kituoni hapo Manji alikuwa bado anashikiliwa.
“Sioni sababu ya kuendelea kushikilia
watu wale bila hatua, kama mimi nilituhumiwa tena kwa kutangazwa, lakini
mwishowe ikabainika hakuna ukweli, nitaamini vipi kama waliobaki ndani mikononi
mwa Polisi nao wanahusika?” Alihoji.
0 comments:
Post a Comment