Charles James
Rais John Magufuli |
SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kutangaza kuwa
Serikali haitatetea Watanzania wanaokamatwa nje ya nchi kwa kufanya biashara ya
dawa za kulevya, baadhi ya wasomi na wanasheria wametoa maoni tofauti kuhusu
kauli hiyo baadhi wakiipinga wengine wakiunga mkono.
Akizungumza wakati wa kumwapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka
ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Dk
Anna Makakala juzi, Rais Magufuli alisema hakuna Serikali inayoweza kutetea
watu wanaojihusisha na biashara hiyo na kumtaka Waziri wa Mambo ya Nje na mabalozi
kuwaacha ili wapate haki zao.
Akitoa maoni yake, Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za
Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema yawezekana Rais alikuwa na
hasira kutokana na kukerwa na namna biashara hiyo inavyoharibu picha ya Tanzania.
Alisema pamoja na kwamba biashara hiyo ni haramu na
imekuwa na athari kubwa kwa nchi ikiwamo kuua nguvukazi ya Taifa ambapo vijana
wengi wameathirika, bado kama Rais anapaswa kuhakikisha raia wake hawapati
adhabu kubwa ambayo hata nchini haitolewi.
“Siungi mkono kusema kama wananyongwa wanyongwe tu,
akumbuke kwamba adhafu ya kifo inakwenda kinyume na sheria ya haki za binadamu
ambayo Tanzania iliisaini sasa utaruhusu vipi wananchi wapate adhabu kali
ambayo hata nchini haitolewi?
“Nchi zingine husaidia raia wao wanapopatwa na adhabu
kali ambayo inakiuka haki za binadamu, ipo kesi miaka ya nyuma ya raia wa
Trinad &Tobago ambaye alihukumiwa kunyongwa nchini lakini Waziri Mkuu wao akaomba wamchukue akaadhibiwe
kwao,” alisema Dk Kijo-Bisimba.
Katika kauli yake Rais Magufuli alisema kama mtu
ameshikwa katika nchi yoyote ambayo sheria yake ni kunyongwa Serikali itamwacha
anyongwe, “nasema hili kwa dhati simung’unyi maneno, kwani tukichekacheka Taifa
letu litaangamia.”
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari
ambaye kitaaluma ni Wakili, alisema Rais Magufuli alitoa kauli hiyo bila kujua
kwamba kuna nchi ambazo tayari zina makubaliano na Tanzania za kubadilishana
wafungwa ili wakahukumiwe kwenye nchi zao.
Profesa Safari alisema kauli hiyo haioneshi kama Rais
anajali wananchi wake kwani kitendo cha kusema mabalozi wasishughulike nao ni
makosa, kwani inawezekana ipo orodha ya Watanzania ambao wanakamatwa kimakosa na
hivyo kukosa msaada wa nchi kuwanusuru.
“Mfano sisi na Mauritius tuna makubaliano ya kubadilishana
wafungwa wetu, sasa kama anasema Serikali haitahusika na kukamatwa kwa raia
wake, ina maana anatoa uhuru kwa nchi zingine kukiuka makubaliano yetu, hii itasababisha
kushuhudia watu wengi wakihukumiwa bila kuhusika kwa sababu Serikali tayari
imeshajitoa,” alisema Profesa Safari.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kitivo
cha Sheria, Dk Onesmo Kyauke alisema inawezekana Rais alizungumza hivyo kuonesha
msimamo wake wa namna gani anapiga vita dawa za kulevya.
“Ukitazama takwimu za raia wa Tanzania waliokamatwa nje
ya nchi wakihusishwa na biashara hii ni kubwa na wengi walikuwa wanapata msaada
kutoka balozi zetu, lakini kitendo cha Rais kusema waachwe kitasaidia kwa kiasi
fulani kupunguza orodha ya Watanzania wanaojihusisha na ‘unga’ ili kulinda sura
ya nchi yetu,” alisema Dk Kyauke.
Rais Magufuli alisema jumla ya Watanzania 1,007
wamekamatwa na kuhukumiwa kunyongwa katika nchi 19 tofauti duniani.
0 comments:
Post a Comment