Mariam Cyprian, Tanga
TAHARUKI iliyojitokeza juzi mbele ya Rais John Magufuli,
kwa mkazi wa Tanga, Swabaha Shosi kudai kudhulumiwa mirathi ya mumewe, imeibua
sintofahamu mpya baada ya waliojiita familia ya huyo mume, kujitokeza na
kutangaza kutomtambua Swabaha.
Akizungumza jana Tanga na mwandishi wa JAMBO LEO,
mwanafamilia aliyejitambulisha kuwa mtoto katika familia hiyo, Saburia Mohamed (37),
alidai mara ya kwanza kumwona Swabaha, ilikuwa siku ya kumaliza msiba wa baba
yake.
Juzi katika kilele cha Siku ya Sheria, Swabaha huku
akilia mbele ya Rais Magufuli na uongozi wa juu wa Mahakama na Polisi, alidai
kunyimwa haki ya mirathi ya mumewe na vyombo vya kutoa haki nchini.
Swabaha ambaye alifanikiwa kugonga vichwa vya habari juzi
na jana, alitaja vyombo vilivyomnyima haki kuwa ni Polisi, Mahakama, Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Lakini jana Saburia, aliyejitambulisha kwa mwandishi wa
gazeti hili kama mwanafamilia, alidai kutomtambua na kueleza kuwa siku ya
kwanza kumwona, ilikuwa ya kumaliza msiba wa baba yao.
Saburia alidai kuwa siku hiyo Swabaha alitambulishwa kama
binamu yao kwa shangazi yao aliyeko Mombasa na alikuwa akitoka eda Dar es
Salaam baada ya kufiwa na mumewe.
"Yule mama sisi kwa mara ya kwanza tulitambulishwa
siku ya kumaliza msiba wa baba yetu tukiwa kwenye kikao cha familia, alifika saa
sita mchana, tukaambiwa kuwa ni mjomba wa marehemu baba na ametoka eda Dar es
Salaam ya aliyekuwa mumewe naye alithibitisha hilo," alidai.
Hata hivyo, Saburia alidai kuwa wakili wa familia
alipokuwa akisoma wosia wa marehemu, Swabaha alimnyang'anya wosia huo na
kukimbia nao baada ya kuona jina lake halimo.
Mtoto huyo alidai kuwa mwaka 2012 ilifunguliwa kesi
ambayo ilimalizika kwa kufutwa Desemba 15, mwaka juzi na mwaka huo huo familia
ilipeleka maombi Mahakama ya Mwanzo, kumpendekeza Saburia awe msimamizi wa
mirathi.
Alidai kabla ya kupewa usimamizi, Swabaha
alijitokeza mahakamani na kupinga kwa madai kuwa anayependekezwa kusimamia
mirathi hiyo si mtoto halali wa marehemu.
Saburia alidai kuwa mama huyo hakuwa sahihi kupeleka
taarifa kwa Rais, kwani kesi yao bado inaendelea Mahakama Kuu, ambako
inasikilizwa na Jaji Amour Said Khamis na bado hukumu
haijatolewa.
Alidai kuwa yeye na familia yake hawana vitisho vyovyote
kwa mama huyo na familia ilipatwa na butwaa aliposema anahitaji ulinzi kwa kuwa
anatishwa.
Mtoto huyo alielezea masikitiko yake kuwa ameumia baada
ya Swabaha kumtangaza mbele ya Rais kuwa anahusika na uuzaji wa dawa za
kulevya, kitu ambacho si kweli na kwamba yuko tayari kufanyiwa uchunguzi wa
jambo hilo.
"Mimi ni mfanyabiashara wa nguo na nina duka langu
la nguo barabara ya 14, ameniumiza sana pamoja na familia yangu kwa kusema nauza
dawa za kulevya. Naomba Serikali iliangalie hili, kwani niko tayari kufanyiwa
uchunguzi wa tuhuma hizi," alidai.
Mbali na Saburia, mwandishi wa habari hii alizungumza na
aliyetambulishwa kuwa mke mkubwa katika familia hiyo, Mariam Juma ambaye alidai
kuwa hamfahamu Swabaha.
"Mimi ninamfahamu mama yake ambaye ni wifi yangu na
anaishi Mombasa, yeye sijawahi kumwona. Sasa nilishangaa kubadilika na kusema
kuwa ni mke wa marehemu na kudai ananyanyasika kwa kudhulumiwa mirathi," alisema
Mariam.
Aliitaka Serikali iingilie kati suala hilo ili wapate
haki zao yeye na familia yake, ambayo ina watoto tisa na wake wawili.
Juzi Rais Magufuli aliwaagiza Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Mkurugenzi wa Mashitaka, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na Mahakama
kupitia Jaji Kiongozi, kushughulikia jambo hilo ikiwa ni pamoja na kuhamishia
kesi hiyo Mahakama ya Juu ili uamuzi ufanyike.
0 comments:
Post a Comment