Fidelis Butahe, Dodoma
Nape Nnauye |
SIKU nne baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda, kuwataja wasanii kadhaa wa muziki wa kizazi kipya na filamu akiwatuhumu
kuhusika kwa namna tofauti na biashara ya dawa za kulevya, Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amesema ni makosa kuwahukumu moja kwa
moja kuwa wanajihusisha na biashara hiyo.
Nape amesema licha ya kuunga mkono juhudi za kupambana na
biashara na matumizi ya dawa za kulevya, busara inapaswa kutumika katika kuwabainisha
watuhumiwa kwa sababu bado hawajahukumiwa na Mahakama.
“Ni muhimu kulinda haki ya mtuhumiwa, jambo lenye mjadala
ni busara inayotumika kushughulika na wahusika ili kusaidia vyombo vingine
kuwataja wanaosambaza,” alisema Nape jana katika mkutano wake na waandishi wa
habari mjini hapa.
“Tusiwahukumu kwa tuhuma maana wasanii kujenga brand (kujenga
jina) ni kazi kubwa ila kubomoa jina ni sekunde tu. Ni sawa na kusema huyu
kichaa, lazima jamii itamchukulia ndivyo sivyo.”
Februari 2 mwaka huu, Makonda aliwataja wasanii kadhaa
pamoja na askari polisi 12 kwa tuhuma za kuhusika na biashara ya dawa za
kulevya. Mpaka sasa takribani wasanii saba wameshahojiwa, huku askari hao
wakisimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi yao.
Wasanii wanaochunguzwa kwa tuhuma hizo ni Khalid Mohamed
(TID), Dogo Hamidu, msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu na Babuu wa Kitaa
ambaye pia ni mtangazaji wa Televisheni ya Clouds.
Wengine ambao wametakiwa kufika kituo Kikuu cha Polisi
kwa ajili ya kuhojiwa ni mwanamuziki, Vanessa Mdee na Tunda Sabasita.
Tangu kuibuka kwa sakata hilo, wadau mbalimbali wamekuwa
wakikosoa utaratibu uliotumika kwa maelezo kuwa wasanii hao wanahukumiwa kabla
ya uchunguzi kufanyika ili ibainike kama wanajihusisha na biashara hiyo ama la.
“Ni vizuri tukaangalia, tufanye katika namna ya kumlinda
mtuhumiwa ili hata kama hausiki jina lake lisiporomoke,” alisema Nape.
“Matumizi ya dawa za kulevya yanaathiri wadau wetu ndio
maana tumekuwa tukifanya juhudi za kuwasaidia kuwapeleka katika vituo maalumu
vya kuwasaidia kuondokana na matumizi ya dawa hizi.”
Mbunge huyo wa Mtama alisema licha ya juhudi za kupambana
na dawa za kulevya, kumekuwa na sintofahamu kuhusu sheria ya dawa za kulevya
kutosema chochote kwa anayetumia.
Alisema wapo watu wa kada mbalimbali wanaotumia dawa za
kulevya, lakini wasanii wanaonekana zaidi kwa kuwa ni maarufu na kubainisha
jinsi Serikali kupitia wizara yake inavyowasaidia kuondokana na matumizi ya
dawa za kulevya, akiwemo msanii Rehema Chalamila maarufu kama Ray C.
“Matumizi ya dawa za kulevya ni tatizo la jamii nzima,
mapambano lazima yaanzie kwenye familia zetu. Hawa watu wanahitaji msaada kama
ilivyo kwa wagonjwa wengine,” alisema Nape.
Alipoulizwa nini suluhisho la utaratibu unaotumika
kuwataja na kuwahusisha moja kwa moja wasanii na biashara hiyo alisema, “tuache
jamii ijadili.”
0 comments:
Post a Comment