SAKATA LA MAKONDA
Waandishi Wetu
Job Ndugai |
SASA ni wazi kuwa Spika Job Ndugai ana
kibarua kizito kuhitimisha kwa vitendo utekelezaji wa maazimio manne ya Bunge,
likiwemo la kuwaita wateule wawili wa Rais kuwahoji kuhusu matamshi yao dhidi
ya mhimili huo wa dola.
Wakati wabunge wamelieleza JAMBO LEO
jinsi wanavyosubiri kauli yake kuhitimisha suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika na Katibu wa
Bunge, Dk. Thomas Kashillilah nao wamemtupia mpira Spika kuhusu suala hilo.
Jumamosi iliyopita Ndugai aliliambia
JAMBO LEO kuwa mwenye mamlaka ya kutoa barua ya wito kwa wateule hao ambao ni Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander
Mnyeti ni Dk. Kashillilah ambaye jana alisema jukumu hilo lipo chini ya Spika.
Kabla ya kauli hiyo, Ndugai alinukuliwa
na gazeti hili Jumatano iliyopita
akisema kuwa anashughulikia jambo hilo na likikamilika atavitaarifu
vyombo vya habari.
Sakata la Makonda na Mnyeti liliibuka
katika Mkutano wa Sita wa Bunge uliomaliza Februari 10 mwaka huu mjini Dodoma,
baada ya mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara kutoa hoja kwamba wateule
hao walitoa matamshi yanayoingilia haki na madaraka ya Bunge.
Katika hoja hiyo, Waitara alisema
Makonda alisema wabunge huwa wanakwenda bungeni kusinzia, kauli ambayo inakiuka
haki za Bunge na kwamba Mnyeti alitumia mitandao ya kijamii kuwaita
wabunge wapuuzi.
Akitangaza maazimio hayo baada ya
kupitishwa na wabunge, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alisema wateule hao
wataitwa kujieleza mbele ya kamati ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge.
“Kamati yetu inafanya kazi kwa maelekezo
ya Spika. Tukipokea maagizo ndio tutakutana na kujadili, “ alisema Mkuchika.
Wakati Mkuchika akieleza hayo, Dk
Kashillilah alisema, “Unataka kufahamu hilo jambo kupitia kwangu? Hayo mambo
muulizeni Spika siyo yangu.”
Licha ya juhudi za kumtafuta Ndugai jana
kugonga mwamba kutokana na simu yake kuita bila majibu, wabunge mbalimbali
walionesha imani kwa Spika huyo na kusisitiza kuwa yeye ndio mwenye jukumu la
mwisho katika utekelezaji wa maazimio hayo.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan
Lyimo alisema baada ya maazimio ambayo wabunge wote waliyapitisha, lilikuwa ni jukumu la Katibu wa Bunge na Spika
kupeleka barua za wito kwa wahusika.
“Siyo kwamba maazimio yale yalipofikiwa
basi wahusika wanapaswa kufika na kujieleza bali inahitaji muda wa kuitwa
lakini pia kukutana kwa kamati ambayo ina wajumbe 18. Wajumbe hawa wanahitaji kupewa
posho kutokana na muda ambao watautumia kuendesha vikao vyao,” alisema Lyimo
ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo.
“Kamati yetu ni tofauti na kamati
nyingine. Sisi tunakutana kwa dharura, inawezekana wahusika wameshapelekewa
barua ya wito lakini Spika kwa busara zake akaona asubiri vikao vya kamati
vikianza ndio iunganishwe moja kwa moja kwa kukwepa gharama za matumizi.”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa
Vwawa (CCM) Joseph Hasunga na kwenda mbali zaidi kuwa wabunge sasa wapo katika
majimbo yao na huenda Spika amelisitisha jambo hilo mpaka vitakapoanza vikao
vya kamati.
“Maazimio yakitolewa yanaenda moja kwa
moja serikalini hivyo ni lazima waitwe haiwezi kupingika. Tusiwe na hofu muda
bado upo na vikao vya kamati vinaanza mwanzoni mwa mwezi ujao, nadhani tutapata
mrejesho,” alisema Hasunga.
Mbunge wa Mkuranga (CCM), Abdallah Ulega
alisema Ndugai hawezi kwenda kinyume na maazimio hayo na kusisitiza kuwa ili
wateule hao wa Rais wahojiwe, ni lazima taratibu zifuatwe.
“Siyo kwamba baada ya maazimio basi nao
wanakwenda bungeni. Bunge lina taratibu zake kila kitu kipo kwa Spika yeye ndio
anatakiwa aite kamati yake ili wawajadili lakini nafikiri anasubiri vikao vya
jumla vya kamati,” alisema.
“Usidhani suala hili limekwisha unapaswa
kutambua kuwa Bunge likishaamuru kitu kifanyike hakuna chombo kingine chenye
uwezo wa kupinga ikiwemo Rais. Hili
suala lipo chini ya Spika yeye ndio anatakiwa ampe oda Katibu wa Bunge,”
alisema Khatib Said haji, mbunge wa Konde (CUF).
“Tusubiri tuone kamati zikianza. Spika
hawezi kupingana na wabunge wake na ninafahamu ameshaanza kuchukua hatua dhidi
ya suala hili hivyo hakuna mabadiliko yoyote.”
Maazimio mengine
Maazimio mengine yaliyopitishwa na Bunge
ni endapo kamati itaridhika kwamba kuna jinai, Mwanasheria Mkuu wa Serikali
awasiliane na vyombo vingine vya kiuchunguzi kufuatilia suala hilo na kuchukua
hatua kwa taratibu za vyombo hivyo.
Vilevuile, Bunge liliazimia kwa kauli
moja kuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), atume
waraka kwa wakuu wa mikoa na wilayta kutoingilia mhimili wa Bunge.
Katika azimio jingine, endapo kamati
hiyo ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itathibitisha tuhuma dhidi
yao, Bunge linaazimia mamlaka ya uteuzi ijulishwe ili kuwawajibisha.
0 comments:
Post a Comment