Suleiman Msuya
WAKALA wa
Barabara Tanzania (Tanroads), umetiliana saini ya ujenzi wa daraja la Ubungo na
Kampuni ya China Civil Engeneering Constraction Corporation (CCECC), ambao
unatarajiwa kuanza mwezi ujao na kugharimu zaidi ya Sh. bilioni 177.
Utiaji saini huo
unakuja siku chache baada ya Rais John Magufuli kumuomba Makamu wa Rais wa
Benki ya Dunia (WB) upande wa Afrika, Makhtar Diop kusaidia ujenzi huo wakati
wa uzinduzi wa usafiri wa mabasi ya mwendokasi.
Mtendaji Mkuu wa
Tanroads, Mhandisi Patrick Mfugale alibainisha hayo alipozungumza na waandishi
wa habari jana baada ya utiaji saini makubaliano hayo makao makuu ya wakala huo
jijini Dar es Salaam, huku ikibainishwa jengo la Makao makuu ya Tanesco
halitaguswa na ujenzi wa daraja hilo la ghorofa tatu.
Mfugale alisema
makubaliano yao ni kuwa ujenzi uanze kuanzia sasa na utadumu kwa miezi 30 ili
kuondoa changamoto ya foleni kwenye eneo la Ubungo.
Alisema WB
imetoa mkopo huo ambapo mkandarasi atalipwa moja kwa moja na Sh. bilioni 8.2
atalipwa mhandisi mshauri kwa ajili ya usimamizi ambaye ni Kampuni ya M/s Dasan
ya Korea Kusini ikishirikiana na Kampuni ya Afrika Ltd ya Tanzania.
"Tumetiliana
saini ujenzi wa Daraja la Ubungo ‘interchange’ na Kamapuni ya CCECC ambapo zaidi
ya Sh.bilioni 177 zitatumika na litakuwa daraja la ghorofa tatu ni kazi ya
miezi 30," alisema.
Mfugale
alisema safu ya chini ya daraja hilo itatumika kwa magari ya Barabara ya
Morogoro na kupinda kushoto na safu ya pili itajengwa katika urefu wa mita 5.75
kutoka usawa wa ardhi na itatumika kwa magari yote yanayopinda kulia na
kuongozwa taa za barabarani.
Alisema Safu ya
tatu itajengwa kwa urefu wa meta 11.5 kutoka usawa wa ardhi na itatumika kwa
magari yanayopita Barabara za Mandela na Sam Nujoma na barabara zote zitakuwa
na njia sita.
Mtendaji huyo
alisema kampuni 48 ziliomba zabuni ila ni 14 ambazo zilirejesha hivyo baada ya
kupitia kwa makini CCECC ilifanikiwa kushinda.
Alisema upembuzi
yakinifu na usanifu wa kina ulifanywa na Kampuni ya M/s Hamza Associates ya
Misri kwa kushirikiana na Kampuni ya Advanced Engineering Solutions Ltd ya
Tanzania kwa gharama ya zaidi ya sh. milioni 951 ambapo kazi ilikamilika
Desemba 2016.
0 comments:
Post a Comment