Hussein Ndubikile
BARAZA
la Mitihani la Taifa (Necta), linatarajia kuanza upimaji maalumu wa stadi na
maarifa kwa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu shule
za Serikali.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyopatikana jana kutoka Necta na kusainiwa na Kaimu
Mtendaji, Dk. Richard Kasuga, makatibu tawala Tanzania Bara wanajulishwa kuanza
kufanikisha mchakato huo na upimaji huo unatarajiwa kuanza Februari 28, mwaka
huu.
Ilifafanua
kuwa wanafunzi wote waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu wanatakiwa
kufanyiwa mtihani maalumu kwa ajili ya kuwapima ili kubaini uwezo wao waliouonesha
katika mitihani yao ya shule ya msingi.
Iliongeza
kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuwabaini wanafunzi waliofaulu kwa njia ya
udanganyifu na watakaobainika wataondolewa shuleni.
“Baraza la Mitihani linawajulisha makatibu
tawala kuwa litafanya upimaji maalumu wa stadi na maarifa kwa wanafunzi
waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za umma, Februari 28,
mwaka huu,” ilisema taarifa hiyo.
Pia
taarifa hiyo iliwataka makatibu tawala wote kuwasilisha idadi ya wanafunzi
waliochaguliwa kidato cha kwanza kwa Katibu Mtendaji wa baraza hilo kabla ya
Februari 10, mwaka huu.
Wakati
huo huo, maofisa elimu wa shule za sekondari na wakuu wa shule za umma walitakiwa
kujulishwa kuhusu mchakato huo ili kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza.
0 comments:
Post a Comment