Leonce Zimbandu
Mohamed Mpinga |
KAMANDA wa Kikosi cha Usalama Barabarani
nchini, Mohamed Mpinga, amewapiga mafuruku abiria kupakiwa kwenye magari yanayosafirishwa
kwenda nje ya nchi yenye namba inayoanza na IT, licha ya kipato duni cha
madereva wake.
Mpinga alisema hayo hivi karibuni jijini
Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha
Madereva na Wadau wa Magari Yaendayo Nchi Jirani (ITDA), uliohudhuriwa na mamia
ya wanachama hao.
Mpinga alisema lengo ni kupunguza ajali
za magari ya IT ambayo hayajasajiliwa rasmi kutoa huduma za usafiri, hivyo
kitendo cha kutoa huduma ni kinyume na sheria za nchi.
Alisema ni wajibu wa kila dereva
kuzingatia sheria za usalama barabara kwa mujibu wa maadili ya udereva, ili
kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
“Unajua ilitokea ajali moja mkoani Morogoro
baada ya gari la IT kugongana na gari lingine, abiria aliyekuwa kwenye gari la
IT alikufa lakini dereva alipata majeraha tu,” alisema.
Mwenyekiti wa ITDA, Jimmy Mwalugelo
alisema wananchama wake wanakabiliwa na changamoto ya mawasiliano kati ya
dereva na mwagizaji, hali inayowafanya kuishi maisha magumu.
Alisema madereva hao hawana ajira wala
mkataba, lakini wanazo leseni za udereva zinawapa sifa ya kuendesha magari
hayo, hivyo itakuwa vyema kwa Serikali kuwatambua rasmi.
“Tunasubiri mpango wa kutumia vibao
vyenye rangi nyekundu, bendera na stika ambayo itakuwa na jina la dereva, ili
kuepuka udanganyifu na kuongeza umakini kwa dereva,” alisema.
Mwakilishi kutoa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Johansen Gaitano, alisema suala hilo la kutambua chama hicho, linapaswa
kushirikisha wadau mbali mbali, wakiwamo waagizaji wakubwa wa magari.
“Iwapo wadau wote watakubali na kutambua
chama cha ITDA itakuwa rahisi katika utekelezaji wake kuliko ilivyo sasa lakini
Serikali tayari imewapokea,” alisema.
0 comments:
Post a Comment