Wanasheria wachanganua tuhuma za ajira kwa Manji


*Ni kuhusu nafasi na uwajibikaji wake Quality Group

Waandishi Wetu
Yusuf Manji
WAKATI Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam ikikusudia kumfungulia mashtaka mfanyabiashara maarufu, Yusufu Manji, kwa tuhuma za kuajiri wafanyakazi wageni 25 wasio na vibali vya kufanya kazi nchini, wanasheria nchini wamekosoa kusudio hilo.

Wamesema wafanyakazi walioajiriwa na kampuni ya Quality Group, kama wanafanya kazi nchini bila vibali wanaopaswa kuulizwa ni watendaji wanaohusika na ajira na si mmliki wa kampuni kwa maelezo kuwa hahusiki.

Wakati juzi Uhamiaji ikitoa maelezo hayo, Julai 15 mwaka jana Manji alitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari, akieleza kustaafu rasmi nafasi yake ya Mkurugenzi Mtendaji wa Quality Group.

Katika maelezo yake kwenye taarifa hiyo, Manji alisema baada ya kustaafu atabaki kuwa mshauri tu, huku akitaja sababu za kufanya hivyo kuwa ni utaratibu uliowekwa na waasisi wa kampuni hiyo, kwa kuwa na ukomo wa uongozi usiozidi miaka 20.

Akizungumzia suala hilo jana, mwanasheria maarufu nchini, Tundu Lissu alisema: “Jambo la kwanza ni makosa na jambo la pili ni kuamua nani mwenye makosa hayo.”

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, alisema kampuni ni mtu kisheria, yanapotokea makosa ya jinai, kampuni haiwezi kufanya makosa hayo bali wanaoiongoza, kuiendesha au kuimiliki.

“Kwa kawaida wanaoendesha kampuni si lazima wawe wanaoimiliki. Unaweza kumiliki kampuni lakini usihusike kabisa katika masuala ya utawala na wala usiwe kwenye Bodi ya Wakurugenzi,” alisema Mwanasheria Mkuu huyo wa Chadema.

“Wanaohusika kwenye makosa ya jinai kama yamefanywa ni wale wanaoiendesha kampuni. Suala la kujiuliza kwenye kampuni za Quality Group ni nani Mkurugenzi Mtendaji wake, Meneja, Ofisa Utumishi na watu wa aina hiyo?”

Akizungumzia wenye hisa katika kampuni hiyo, alisema: “Unaweza kukuta mwenye hisa alikuwa au yuko Marekani sasa utasema amefanya kosa la kuajiri wafanyakazi wasio na vibali Tanzania? Kitu muhimu ni kuangalia nani anayeendesha kampuni kwa sasa.

“Kuna uwezekano mkubwa kuwa anayemiliki akawa anaiendesha na inawezekana anayeimiliki akawa haiendeshi.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse alisema kulingana na suala hilo la uhamiaji, si sahihi kuhusisha mmiliki moja kwa moja.

Wakati sakata la Manji likishika kasi, hivi karibuni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Viongozi wa Dini, Askofu William Mwamalanga alinukuliwa na gazeti moja la kila siku akizungumzia ukumbi wa Bilicanas uliokuwa ukimilikiwa na kampuni ya Mbowe Hotels ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Katika maelezo yake, Mwamalanga alisema ukumbi huo ambao umeshavunjwa ni moja ya maeneo yanayotumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kufanya biashara zao, lakini si mwanasiasa huyo ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Katika maelezo yake, Dk Jesse alisema: “(Manji) anaweza kuwafungulia kesi upande wa mashitaka.”

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo hicho, Kitivo cha Sheria, Dk Onesmo Kyauke alisema, “Hapana hawezi kushtakiwa mmiliki. Huyo anayeiendesha ndiyo mwenye dhamana ya kujibu hayo yote.”

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema: “Kwa mujibu wa sheria za kampuni sura ya 212 wanaowajibika ni wakurugenzi…, hata hivyo nimeshangazwa na mambo mawili:

“Kwanza, kuandamwa kwa mmiliki mmoja tu na kwa mujibu wa sheria, kampuni haiwezi kumilikiwa na mtu mmoja. Pili, kiwango cha matangazo kwa suala hili ambalo ni la kiuhamiaji kana kwamba ni mauaji!”

Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stola alisema: “Inategemea na hatua ambayo mhusika atakuwa amejitoa katika kampuni hiyo kama si sahihi au kama ana hisa.

‘’Umiliki ni kuwa na hisa, ikiwa atakuwa amejitoa bila kuondoa hisa zake, jambo lolote likitokea katika kampuni, watu wote wenye hisa watahusika, lakini pia itategemea na kosa kama litakuwa la jinai au madai.”

Profesa Abdallah Safari alisema: “Kama hana hisa kwenye kampuni hawezi kuhusishwa. Wenye hisa wote kampuni ikishtakiwa wanakuwa na la kujibu ila kama hana hisa hawezi kushtakiwa kwa lolote.”

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo