Abraham Ntambara
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezindua elimu
kwa umma kuhusu huduma ya kuhama kutoka mtandao mmoja wa simu kwenda mwingine
bila kubadili namba ya simu ya kiganjani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jana Dar es Salaam, Mkurugenzi
Mkuu, James Kilaba alisema huduma hiyo itamuwezesha mteja kubaki na namba yake
bila kujali mtandao anaotumia, kwani anapoamua kuhama huhama nayo kama ilivyo.
“Mteja hana haja ya kusumbuka kuwataarifu watu wake wa
karibu, marafiki, familia na wafanyakazi wenzake au washirika katika shughuli
zake kwamba amebadilisha namba kwani inabakia ile ile,” alisema Kilaba.
Aidha alisema huduma hiyo kwa Bara la Afrika imeanzishwa pia
nchini Misri, Kenya, Sudani, Afrika Kusini, Ghana, Nigeria, Senegal na Morocco.
Aliongeza kuwa nchi za Rwanda, Namibia na nyinginezo zipo
katika mchakato wa kuanzisha huduma hiyo pia.
Kilaba alifafanua kuwa uanzishwaji wa MNP ni kwa mujibu
wa kanuni za mwaka 2011 (Electronic and Postal Communications) Regulations,
2011) za uanzishwaji wake ambapo alisema kuwa kanuni hizo zinawataka watoa
huduma za simu za kiganjani kuwezesha huduma hii katika mitandao yao.
Alisema katika utekelezwaji wake, TCRA imewashirikisha
watoa huduma za kibenki ili wafunge mifumo itakayotambua namba zilizohama na
hivyo kuwa na uwezo wa kutuma fedha mitandaoni bila shida yoyote.
Kilaba alisema faida za huduma hii ni nyingi, ikiwamo kuongeza
ushindani kwenye sekta ya mawasiliano na hivyo kuwa kichocheo cha utoaji huduma
bora kwani bila huduma nzuri wateja watahama.
Aliongeza nyingine ni kumpa uhuru mtumiaji wa huduma za
simu za viganjani kuchagua mtoa huduma ambaye anaona anatoa huduma bora Zaidi.
Alisema TCRA imeandaa program ya kuelimisha wananchi juu
ya mfumo huu ambapo elimu hii itafanyika kupitia vipindi vya redio, televisheni
na kwa njia ya vipeperushi mbalimbali.
Alisema kupitia vipindi hivyo wananchi wataelimishwa
namna ya kuhama pamoja na vigezo na masharti yake. Pia wataelimishwa haki zao
wakati wa kuhama.
0 comments:
Post a Comment