Grace Gurisha
Paul Makonda |
HATUA ya kutaja hadharani majina ya watu wanaodaiwa
kutumia na kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, imechukua sura mpya
baada ya Mahakama Kuu nchini kuwaita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro.
Mwingine aliyetakiwa kufika mahakamani hapo leo ni Mkuu
wa Upelelezi wa kanda hiyo (ZCO) Kamilius Wambura, huku taarifa zikibainisha
kwamba viongozi hao wamepelekewa mwito wa kufika mahakamani hapo kutokana na
kesi yaKikatiba iliyofunguliwa dhidi yao na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Kesi hiyo ya Mbowe ni namba moja ya mwaka 2017, imepangwa
kutajwa leo, ambapo pamoja na mambo mengine anapinga mamlaka ya Makonda
kumkamata na kudhalilisha watu.
Katika kesi hiyo Mbowe anaiomba Mahakama itamke kuwa vifungu
vya Sheria ya Tawala za Mikoa vinavyowapa mamlaka wakuu wa mikoa na wakuu wa
wilaya kuwakamata watu na kuwatia mbaroni, viko kinyume cha Katiba.
Jopo la majaji watatu litasikiliza kesi hiyo akiwamo,
Sekieti Kihiyo (Mwenyekiti wa jopo), Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia
Kaday.
Hata hivyo taarifa zaidi zinaeleza kuwa mwito huo wa
Mahakama haukupokelewa na Makonda wala Wambura, ikielezwa hawakuwepo ofisini na
wasaidizi wao walikataa kusaini ili kuzipokea huku Kamanda Siro akidaiwa
kukataa kupokea mwito huo.
Ofisa wa mahakama aliyepeleka mwito huo, Yusuph Juma,
baada ya kuelekezwa na Kamanda Sirro kuwa ampelekee mwito huo Wambura,
alipokwenda kwa Wambura, hakumkuta.
Kwenye hati hiyo ya mwito kwenda kwa Kamanda Siro, Juma
aliandika: “Kwa hiyo wito haujapokelewa.”
Katika hatua nyingine jana Mbowe ambaye pia ni Kiongozi
wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alifungua maombi mengine mahakamani hapo akipinga
kusudio la Kamanda Siro la kumkamata kama hatajisalimisha katika kituo cha
Polisi kwa mahijiano.
Katika maombi hayo namba 21 ya mwaka 2017, Mbowe anaiomba
Mahakama iwazuie wadaiwa kutekeleza azma yake ya kumtia mbaroni pamoja na mambo
mengine akidai kuwa kuna kesi ya kikatiba ambayo tayari ameifungua mahakani
hapo.
Hivyo aliiomba Mahakama itoe amri ya kuwazuia kumkamata
hadi hapo kesi hiyo ya kikatiba itakapomalizika na kwamba Mahakama Kuu imwachie
na Polisi wasiendelee na mchakato wowote dhidi yake hadi hapo kesi hiyo
itakapomalizika.
Katika kesi ya msingi ya Kikatiba, Mbowe anapinga kitendo
cha Polisi kumtaka afike kituoni kwa madai kuwa ni utekelezaji wa amri ya Mkuu
wa Mkoa.
Alidai kuwa sheria inayompa Mkuu wa Mkoa mamlaka ya kutoa
amri ya kumkamata na kumweka ndani mtu, yako kinyume cha Katiba kwa madai kuwa
ilitungwa katika mazingira ambayo hapakuwa na vituo vya Polisi vya kutosha.
Hivyo alidai kuwa kwa mazingira ya sasa sheria hiyo
imeshapitwa na wakati na anaiomba Mahakama itamke kuwa ni kinyume cha Katiba.
Hata hivyo alisema kuwa hata kama Mkuu wa Mkoa alikuwa
anatekeleza mamlaka yake kwa mujibu wa sheria hiyo, basi hakutimiza matakwa ya kisheria,
ambayo ni pamoja na kutoa taarifa kwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya au ya Hakimu
Mkazi.
Hivyo aliiomba Mahakama kama itaona kuwa Mkuu wa Mkoa
alikuwa sawa kutoa amri hiyo, basi imwamuru afuate matakwa ya kisheria, ikiawa
ni pamoja na kulinda haki za binadamu katika kutekeleza madaraka yake hayo.
0 comments:
Post a Comment