Mwandishi Wetu, Dodoma
Pascal Haonga |
MBUNGE wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga, amehoji bungeni
juu ya kutoweka kwa Ben Saanane, ambaye ni msaidizi binafsi wa Mwenyekiti wa
chama hicho, Freeman Mbowe, na kutaka Serikali kueleza alipo.
Saanane alitoweka tangu Desemba mwaka jana na taarifa
zake ziliripotiwa kituo cha Polisi Tabata jijini Dar es Salaam, ambapo hata familia
yake ililieleza kuwa baada ya kumtafuta katika maeneo mbalimbali bila
mafanikio, wameviachia vyombo vya dola kumfatuta.
Huku akitumia kanuni ya 68 (7) jana bungeni, Haonga
aliomba mwongozo huo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, akihoji suala hilo,
lakini uligonga ukuta kwa maelezo kuwa jambo hilo halikutokea bungeni siku ya
jana.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, Saanane amepotea, hajulikani
alipo lakini Serikali haioneshi jitihada zozote kama inavyofanya katika suala
la kumtafuta Faru John,” alisema.
Huku akihoji nani mwenye faida kati ya faru John na
Saanane, Haonga alisema hata Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba,
yuko kimya juu ya kutokewa kwa msaidizi huyo wa Mbowe.
Akitoa maelezo ya mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge,
Andrew Chenge alisema: “Nadhani Haonga ulikuwa unataka kusikika tu, kwanza
huyo Saanane sisi hatumjui, lakini Kanuni ya 68 (7) hairuhusu jambo hilo. Faru
John sijui Saanane sijui ni kitu gani.”
0 comments:
Post a Comment