Mwandishi Wetu, Simanjiro
James ole Millya |
MBUNGE wa Simanjiro, James ole Millya (Chadema) amepongeza
viongozi wa Serikali kwa jinsi wanavyojali na kuhudumia wananchi.
Alitoa pongezi hizo juzi kwenye mikutano miwili ya
hadhara Orkesumet na Mirerani wilayani hapa, baada ya kupewa nafasi kusalimia
wananchi kabla Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hajazungumza nao.
“Serikali hii ina viongozi wachapakazi akiwemo Waziri
Mkuu. Kwa mara ya kwanza katika jimbo hili, wananchi watapata maji safi kupitia
mradi wa maji kutoka Mto Ruvu unaoendelea kujengwa sasa,” alisema akiwa
Orkesumet.
Alitumia fursa hiyo kumwomba Waziri Mkuu afuatilie ujenzi
wa hospitali ya wilaya, kwani sasa wanategemea kituo cha afya na hali ikibadilika
inabidi mgonjwa apelekwe Arusha Mjini umbali
wa kilometa 150 kutoka hapo yalipo makao makuu ya wilaya.
Pia aliomba ijengwe barabara ya lami kuunganisha wilaya
hiyo wilaya za Hai na Kiteto.
Akiwa Mererani, Ole Millya aliipongeza Serikali kwa
kujenga barabara ya lami kutoka uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) hadi Mererani.
Hata hivyo, aliiomba Serikali iongeze juhudi ili barabara hiyo iweze kufika Mirerani
na Orkesumet.
Akijibu maombi hayo, Waziri Mkuu Majaliwa alimpongeza Mbunge
huyo kwa uungwana wake wa kutambua juhudi za Serikali kwa wananchi wa jimbo
lake.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara
yake mkoani Manyara, aliwaambia wakazi hao kwamba Serikali itaendelea kufanya
nao kazi bila kubagua kwa itikadi za kisiasa.
“Mmempa dhamana ya kuwawakilisha kama Mbunge wenu, lakini
dhamana ya kuongoza nchi mmempa Rais John Magufuli kwa kuwapigia kura. Kwa
hiyo, kazi yetu ni kuwatumikia ili tutatue kero zinazowakabili wana Simanjiro,”
alisema.
Akizungumzia sekta ya afya, Waziri Mkuu alisema kituo cha
afya cha Orkesumet kimepewa Sh milioni 49 kati ya Sh milioni 57 zilizoombwa ili
kukiimarisha katika utoaji huduma za tiba.
“Tumeshatuma fedha zingine Sh milioni 163 kati ya Sh
milioni 190 zilizoombwa ili kununulia dawa, vifaatiba na vitendanishi. Pia kuna
Sh milioni 483 zimetengwa kuimarisha huduma za afya vijijini,” alisema.
“Nia yetu ni kujenga hospitali kubwa ya wilaya, lakini ni
lazima tuimarishe miundombinu ya utoaji tiba ili wananchi wapate huduma
stahiki. Ombi la hospitali ya wilaya
nimelipokea na nitafuatilia kujua limefikia hatua gani,” aliahidi.
Kuhusu ujenzi
wa barabara za kuunganisha wilaya, Waziri Mkuu alisema Serikali itaanza
upembuzi na usanifu wa kina wa ujenzi wa barabara ya Arusha – Kiteto – Kongwa,
ili ijengwe kwa kiwango cha lami.
Kuhusu
migogoro ya ardhi iliyotajwa na wananchi kwenye mabango yao, Waziri Mkuu
alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula aende na Mbunge huyo
kwenye maeneo yanayolalamikiwa na wananchi ili kubaini kiini cha migogoro na aipatie
ufumbuzi.
Kuhusu umeme,
Waziri Mkuu alisema vijiji 18 kati ya 57 vya wilaya vimepewa umeme na
vilivyokuwa vimeshaingizwa kwenye mpango wa Serikali wa kuvipatia umeme vijiji
8,000.
Alionya wakazi
wa Mirerani akiwataka wachukue hadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI,
kwani takwimu zinaonesha kuwa kasi ya maambukizi katika mji huo ni asilimia 18
kiwango alichosema ni kikubwa kuliko cha kitaifa.
0 comments:
Post a Comment