BUNGE limeagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutoa maelezo kwa chombo hicho cha kutunga sheria baada ya kutoa kauli zinazodaiwa kuridharau Bunge.
Wakati Bunge likiagiza jambo hilo, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) na Ester Bulaya (Bunda-Chadema), walisema Makonda anapaswa kutambua kuwa uchunguzi unapaswa kufanyika kwanza kabla ya wahusika kutajwa, kusisitiza kuwa taratibu za kisheria zinapaswa kufuatwa.
Uamuzi huo wa Bunge ulitolewa jana na Mwenyekiti wake, Andrew Chenge baada ya mbunge wa Mkuranga (CCM), Abdallah Ulega kuomba mwongozo, akieleza kuwa Makonda wakati akitaja majina ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya jana, alitoa kauli za kuwadharau wabunge kuwa wanalala tu bungeni.
Hoja ya mbunge huyo iliungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge, huku Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini-Chadema), akisema lengo ni kurejesha hadhi ya mhimili huo muhimu katika maendeleo ya nchi.
“Naagiza Ofisi ya Katibu wa Bunge wamtake Makonda atoe maelezo yake kama kweli amesema maneno hayo, watapokea maelezo yake kama hakusema au amesema, yale maelezo yatapokelewa na katibu wa Bunge na atayapeleka kwenye kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge,” alisema Chenge.
“Hapo tutakuwa ndani ya taratibu zetu za kanuni na ndani ya sheria yenyewe ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge maana lazima ithibitike kama kweli imeangukia miongoni mwa haki za Bunge ambazo zinazopaswa kuheshimika.”
Katika mwongozo huo, Ulega alisema wabunge wamekuwa mstari wa mbele kumsaidia Rais John Magufuli katika vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya huku sheria ya kupambana na biashara hiyo ikiwa imepitishwa na chombo hicho.
“Leo wabunge wameambiwa kwamba hawana jambo isipokuwa wanakuja kulala katika Bunge hili, mheshimiwa mwenyekiti mimi ni kijana mzalendo na Makonda ni mdogo wangu na rafiki yangu pia,” alisema Ulega.
“…,Bunge kama chombo huru kiendelee kuheshimiwa na sisi tunadhani kuna mambo mawili, aidha kijana mwenzangu (Makonda) hakuwa anajua anachokisema, au amefanya dharau makusudi.”
Ulega alisema kwa kuwa wabunge ndio watu wa kwanza kumsaidia Rais, alimuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kama mtendaji mkuu wa Serikali kuchukua hatua ili kulinda hadhi ya Bunge na kusisitiza kuwa Makonda atumie vyombo vya havari kuwaomba radhi wabunge na Bunge kwa kauli yake hiyo.
Akijibu mwongozo huo Chenge alisema licha ya kutosikiliza alichokizungumza Makonda, alisema suala hilo hatolipeleka kwa Waziri Majaliwa na wala kumtaka kuomba radhi kwa kuwa hakumsikia alichokisema, kubainisha kuwa Bunge lazima liheshimiwe.
“Kitu chochote ambacho kinakaribia au kinaonekana kudharau au kushusha hadhi ya Bunge hili hakikubaliki hata kidogo,” alisema Chenge.
“Bunge kama taasisi na wajumbe wake na mhimili miongoni mwa mihimili mitatu, lazima liendelee kuheshimiwa na mtu yoyote. Unawea usinipende mimi lakini Bunge liheshimiwe.”
Alisema Bunge katika umoja wake kama taasisi lazima lilinde mamlaka iliyonayo, “Lakini kwa vile tumejiwekea utaratibu wetu kupitia kanuni za Bunge na tuna Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili sasa ikathibitike ameyasema hayo, ameyasema wapi, lini na kama yanaangukia ndani ya sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge. Huko ndiko ukweli wote ukakapodhihirika.”
Huku akiwa makini mbunge huyo wa Mariadi alisema, “narudia tena hiki chombo (Bunge) lazima kiendelee kuheshimiwa na wananchi wote na sisi wenyewe kama wabunge wa chombo hiki lazima tuishi na matendo yetu yaendane na mhimili huu.”
Kauli za wabunge
Akizungumzia suala hilo Bulaya alidai alipigiwa simu juzi na Makonda ambaye alijitamba kuwa anaaminiwa na Rais Magufuli na atawachafulia hadhi wabunge na kwamba atawawekea dawa kulevya wasanii waliokamatwa kwa tuhuma za kufanya biashara za dawa za kulevya ili kuwataja wenzao.
“Huwezi kutaja watu bila kuwa na ushahidi. Makonda ajibu tuhuma za kutowajata wanawake wake ambao wanafanya biashara za dawa za kulevya,” alisema Bulaya.
“Nimewaonesha wabunge namba za simu aliyopiga Makonda ambaye pia Matiko (Ester-Mbunge Tarime Mjini). Amekwenda nje ya nchi na anajitamba Rais anamuamini, sisi tutamueleza Rais mambo ambayo Makonda anayafanya”
Kwa upande wake Zitto alisema, “Mambo haya lazima yaende kwa mujibu wa taratibu na mifumo ya haki si kwa mtu mmoja kuonekana kila kitu. Mbowe (Freeman-Mwenyekiti Chadema) ametajwa na Makonda kuwa anajihusisha na biashara hii. Mbowe ni kiongozi wa upinzani.”
Alisema kinachotokea sasa ni vita ya kisiasa na uamuzi wa Makonda kuwakamata wasanii uliwalenga wapinzani, “Kwa kutaja kule jina la Mbowe limechafuka, zilipaswa kufuatwa taratibu kwa uchunguzi kufanyika na kisha watuhumiwa kupelekwa mahakamani.”
Alisema kutajwa kwa wafanyabiashara bila kuchunguzwa, akiwemo Yusuf Manji ambao wana uwekezaji mkubwa nchini inakuwa ni taabu kuwasafisha ikibainika kuwa hawajihusishi na biashara hiyo.
0 comments:
Post a Comment