Suleiman Msuya
Swabaha Mohamed mbele ya JPM |
MWANAMKE mkazi wa Tanga, Swabaha Mohamed,
amezusha taharuki kwenye sherehe za Siku ya Sheria kwa ‘kufunguka’ mbele ya
Rais John Magufuli akidai kunyimwa haki na vyombo vya kutoa haki nchini kuhusu
mirathi yake.
Mwanamke huyo aliibuka muda mchache
baada ya Rais Magufuli ‘kuwatolea uvivu’ baadhi ya viongozi wa vyombo hivyo;
Polisi, Mahakama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)
kuwa zinashindwa kufanya kazi kwa pamoja.
Swabaha ambaye alikaa viti vya nyuma
akionekana mtulivu na kufuatilia hotuba ya Rais, mwishowe alisimama akiwa na
bango la kitambaa lenye maandishi yakisema vyombo hivyo vinamnyima haki.
Kitendo cha Swabaha kilishitua watu wakiwamo
wa Usalama hasa alipoelekea mbele ili
Rais asome ujumbe wake, ndipo mmoja wa watu wa Usalama alipomfuata na kumrejesha
eneo lake.
Hata hivyo mwanamke huyo alionesha kupinga
ndipo ofisa mwingine akaongeza nguvu na kumrejesha kwenye kiti chake huku
maofisa wengine wawili wakiongezeka na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam, Simon Sirro kuungana nao kumdhibiti.
Baada ya Rais kuona hali hiyo, aliamuru
mwanamke huyo aachwe na apewe nafasi ya kueleza anachotaka akiwa karibu naye,
maofisa hao walimruhusu huku wakimtaka aende bila nyaraka zake.
Kitendo cha kumtaka aache nyaraka
kilimfanya apayuke na Rais akaagiza nyaraka hizo apewe na baada ya kupewa akaelezea
kinachomsibu.
Swabaha alimweleza Rais kuwa kwa
takribani miaka minne anafuatilia haki yake ya mirathi ila kuna watendaji wa
Serikali wanakwamisha kwa makusudi.
Alisema baada ya mumewe kufariki dunia
mwaka 2012 walijitokeza watu wakiwamo wanawake aliozaa nao, mmoja ni mpangaji
wake aliyemtaja kwa jina la Alfred Akaro na mwanawe wa nje, wakishirikiana na
wakili wa Serikali aliyemtaja kwa jina moja la Rebeca kutaka kumdhulumu haki
yake ya mirathi.
Alisema mumewe alioa wake wawili ambao
ndio wanastahili kupata mirathi kwa mujibu wa wosia alioacha, lakini katika
mazingira ya kutatanisha, kundi hilo lilitengeneza nyaraka bandia ili
kuwadhulumu.
Mjane huyo alisema amefikisha malalamiko
yake kwenye vyombo vya ngazi ya juu huku
akikumbana na vikwazo katika baadhi ya ofisi.
“Nimehangaika sana kuhusu hili suala,
ila kuna watumishi wa Serikali wanatumia kila mbinu kunidhulumu wakishirikiana
na kundi la watu, hata Rais nilimtumia ujumbe akamtumia IGP,” alisema.
Swabaha alisema amepigania haki hiyo kwa
muda mrefu hivyo kwa sasa anachotaka ni haki yake au afungwe, kwani anapokea
vitisho kutoka kundi hilo kila kukicha na ujumbe ambao anatumiwa amekuwa
akimtumia IGP.
IGP Ernest Mangu alikiri kupokea
malalamiko hayo na kuwa kuna changamoto kidogo kwa kinachooneka kuwa ni suala
la kifamilia na alimwelekeza Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) Boaz alifanyie
kazi katika kipengele cha jinai.
Katika kuhitimisha hilo, Rais Magufuli
aliwaagiza AG, DPP, IGP na Mahakama kupitia kwa Jaji Kiongozi, Ferdinand
Wambali kuhamishia kesi hiyo Mahakama ya juu ili uamuzi ufanyike.
Aidha, Rais Magufuli alitoa agizo kwa Polisi
kumlinda mwanamke huyo ili asije kudhuriwa na wabaya wake.
0 comments:
Post a Comment