Celina Mathew
Yusuf Manji |
MSHAURI Mkuu wa
Kampuni za Quality Group, Yusuph Manji, jana aliripoti kwenye Kituo Kikuu cha Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kama alivyoahidi juzi kutekeleza agizo la Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Manji alikwenda
kituoni hapo kutokana na ahadi aliyoitoa juzi kwenye mkutano na wanahabari
jijini humo, muda mfupi baada ya Makonda kumtaja akimtuhumu kuhusika na
mihadarati kwenye mkutano wake na vyombo vya habari.
Manji ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, aliwasili kituoni hapo saa
10:55 asubuhi akifuatana na wasaidizi wake wawili na wanasheria kadhaa.
Hata hivyo, gari
lake lilizuiwa kuingia ndani ya eneo hilo, hivyo kulazimika kushuka na kutembea
kuelekea ndani ya kituo hicho.
Wakati Manji akiingia,
polisi waliimarisha ulinzi wa askari na gari la washawasha lililoegeshwa barabarani,
huku baadhi ya watu wanaoaminika kuwa mashabiki wa Yanga wakitanda karibu kila
kona ya eneo hilo.
Saa 5:29 Manji
alitoka ndani ya kituo hicho na kusubiri hadi saa 6 mchana alipoingia tena
ndani kwa mahojiano akiwa na wanasheria wake.
Saa 6:09 alitoka
akiwa na wanasheria wake, lakini alipofika langoni kuelekea kwenye gari, askari
mmoja alitoka ndani haraka na kumwomba arudi ndani.
Manji alitii na kurudi
ndani ambako alihojiwa huku taarifa zikionesha kuwa wakati hayo yakiendelea si Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro wala Makonda aliyekuwapo.
Nje
Wakati Manji
akiendelea kuhojiwa, baadhi ya wananchi walikuwa nje wakimsubiri lakini polisi
waliwatawanya ili eneo hilo libaki wazi kutokana na wingi wao.
Wananchi
Baadhi ya
wananchi walilaani hatua ya Makonda kutuhumu watu kwa kuwataja majina na
kuwaita kupitia vyombo vya habari, badala ya mfumo rasmi kupitia mwito wa Polisi.
Wengine walimpongeza
Manji kwa kwenda kuripoti kabla ya siku husika (leo) wakieleza kuwa alionesha utiifu
bila shuruti.
Mkazi wa Keko, Temeke,
Francis John alisema kitendo alichofanya Manji kwenda Polisi jana bila kusubiri
siku ya mwito, kinapaswa kuigwa na viongozi wengine kwenda kusikiliza
walichoitiwa.
"Kwa kweli
Manji amefanya kitendo cha kiungwana nampongeza kwa kuwa shupavu, namsihi
aendelee na moyo huo huo," alisema.
Salma Hamdani wa
Magomeni, Kinondoni, alisema hatua hiyo ya Manji kuonesha kujali kwa kujitokeza
Polisi inafundisha unyenyekevu na utii, lakini akasema viongozi wa Serikali
wanapaswa kufuata taratibu, sheria na kuzingatia haki za binadamu katika
kuteleza majukumu yao.
Ilipofika saa
10.27 jioni Manji na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Ujima, Josephat Gwajima
waliondolewa kituoni hapo kwa gari Toyota
Land Cruiser nyeupe namba T213ARS na kupelekwa kusikojulikana.
0 comments:
Post a Comment