Sharifa Marira, Dodoma
Jenister Mhagama |
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti
ya Utumishi wa Umma) Angelah Kairuki, amesema Serikali imeondoa kwenye mfumo wake
wa ajira, watumishi hewa 19,629 ambao kama wangelipwa mishahara kwa mwezi,
wangesababisha hasara ya Sh bilioni 19.749.
Kairuki alisema hayo jana wakati akijibu
swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Maida Hamad Abdallah
(CCM) bungeni jana.
Maida alitaka kujua kiwango cha hasara
iliyosababishwa na watumishi hao, ambacho kilibainika kutokana na uhakiki wa watumishi
hewa na hatua za Serikali dhidi ya waliosababisha uwepo wa watumishi hao.
“Ningetoa takwimu ya hasara kwa ujumla,
lakini ingawa tumeshazipata sijakamilisha kufanya hesabu za majumuisho, hivyo
naweza kutoa mifano michache tu kwa kueleza hali ilivyo katika baadhi ya
halmashauri na wilaya,” alisema.
Alisema wilaya ya Kinondoni, ilikutwa na
watumishi hewa 107 ambao walishalipwa Sh bilioni 1.279 huku Halmashauri ya
Kishapu ikikutwa na watumishi hewa 73 ambao walishatafuna jumla ya Sh milioni 543.
Akiuliza swali, Maida alihoji ikiwa
pamoja na hatua zinazochukuliwa dhidi ya walioisababishia hasara hiyo, Serikali
haioni umuhimu wa watu hao kutakiwa kurejesha fedha zilizopotea?
Akijibu, Kairuki alisema katika mashauri
38 yaliyofikishwa mahakamani na kuhukumiwa, wahusika walitakiwa ama kulipa
faini au kurejesha fedha zilizopotea na wanaoshindwa kutekeleza hayo, wanapata
adhabu ya kifungo jela.
Alisema majalada 126 yanaendelea
kushughulikiwa na serikali inaendelea kuchukua hatua dhidi ya kila anayebainika
kuhusika kwa namna yoyote na uwepo wa watumishi hewa serikalini.
Mbunge huyo katika swali lake la msingi,
alihoji kauli ya Serikali juu ya waliohusika
kurudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa njia ya kusababisha uwepo wa watumishi
hewa.
Kairuki alisema hadi Oktoba 25 watumishi
1,663 kutoka wizara, idara zinazojitegemea, wakala za Serikali, sekretarieti za
mikoa na mamlaka za serikali za mitaa walibainika kusababisha hali hiyo.
Alichanganua kwamba kati ya watumishi
hao, 16 ni wa wizara, tisa idara zinazojitegemea
na wakala wa Serikali, sita wa sekretarieti za mikoa na 1,632 wa mamlaka za
serikali za mitaa.
“Hadi siku hiyo (Oktoba 25), jumla ya
watumishi 638 walikuwa wamefunguliwa mashitaka Polisi, 50 wanafanyiwa uchunguzi
na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na 975 wameshitakiwa
kwenye mamlaka zao za kinidhamu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment