Abraham Ntambara
Rais Edgar Lungu |
RAIS
wa Zambia, Edgar Lungu, anatarajiwa kuwasili nchini keshokutwa kwa ziara ya siku
tatu ambapo pamoja na mambo mengine, atatembelea Reli ya Tazara na Bomba la
Mafuta (Tazama).
Katika
ziara hiyo ya kiserikali, Zambia na Tanzania zinatarajiwa kusaini mikataba
minne ya ushirikiano ya kuboresha namna bora ya ufanyaji kazi wa Tazara na Tazama.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda, Dk
Augustine Mahiga aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam, kwamba
Rais Lungu anatarajiwa kuanza ziara hiyo Novemba 27 na atakuwa nchini hadi Novemba
29.
“Rais
John Magufuli, ametoa mwaliko kwa Rais Edgar Lungu wa Zambia na tunatarajia
kuupokea ugeni huo Novemba 27, Jumapili hii. Atatembelea vituo vikuu viwili
vinavyotuunganisha, Tazara na Tazama,” alisema Dk Mahiga.
Alisema
madhumuni ya ujenzi wa Reli ya Tazara yalikuwa ni kwa ajili ya maendeleo ya
kiuchumi ya nchi hizo mbili pia kusaidia ukombozi kwa nchi za Kusini mwa Afrika
na ndiyo sababu ilijulikana kama Reli ya Uhuru.
Aidha,
aliongeza kuwa kwa upande wa bomba la mafuta lilijengwa ili kuirahisishia Zambia
kusafirisha mafuta kutokana na ugumu uliokuwepo baada ya kuwekewa vikwazo na Afrika
Kusini.
“Kutokana
na vikwazo ambavyo Zambia iliwekewa na Afrika Kusini, Mwalimu Julius Nyerere na
Dk Kenneth Kaunda wakajenga hili bomba ili kuepuka vikwazo,” alisema Dk Mahiga.
Alisema
pia Rais Lungu atatembelea kisima cha kuhifadhi mafuta ghafi na kwamba anaamini
ujio wake utasaidia kutatua changamoto zinazokabili Tazara na Tazama.
Waziri
Mahiga alisema kabla ya kumaliza ziara, Rais Lungu atatembelea bandari ya Dar
es Salaam kuangalia sehemu ambako mizigo ya Zambia huhifadhiwa kabala ya
kusafirishwa kwa barabara.
Balozi
wa Tanzania nchini Zambia, Grace Mujama alisema matarajio ya Zambia ni kwamba
baada ya changamoto za bandari ya Dar es Salaam na Reli ya Tazara kutatuliwa, wafanyabiashara
watarudi, kwani waliihama bandari ili kutafuta urahisi wa usafirishaji mizigo.
“Wazambia
walihama Bandari ili kutafuta urahisi wa usafiri, inabidi kuangalia namna ya
kuboresha ili warudi,” alisema Grace.
Balozi
Samwel Shelukindo ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Wizara ya Mambo ya
Nje, alisema mbali na mikataba hiyo minne itakayosainiwa wataweka utaratibu wa
ushirikiano katika sekta ya Uhamiaji, Magereza na Ushirikano kwenye usafiri wa
anga.
“Tutasaini
makubaliano pia ya ushirikiano katika sekta ya Uhamiaji na Magereza, kwa mfano
kuna Watanzania waliofungwa Zambia na pia Wazambia wapo hapa, pia tutakubaliana
juu ya ushirikiano kwenye usafiri wa anga,” alisema Shelukindo.
0 comments:
Post a Comment