Salha Mohamed
Daraja la Kigamboni |
MKUU wa Wilaya
ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, ameiomba Serikali kuangalia upya tozo za magari
ya watumishi wa umma katika Daraja la Nyerere lililoko Kigamboni jijini Dar es
Salaam.
Alitoa ombi hilo
jana wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda kuangalia na
kutatua changamoto za mkoa huo katika wilaya zake mbalimbali.
Mgandilwa
alisema kitendo cha magari ya halmshauri hiyo na watumishi wa umma
wanaoishi nje ya halmshauri kutozwa fedha kwa ajili ya kuvuka katika daraja
hilo, kinaleta changamoto kubwa na kukwamisha ufanisi.
Alimwomba
Makonda kuingilia kati suala la gharama hizo na kuitaka NSSF kuangalia
upya tozo kwa magari yote ya halmshauri na magari binafsi
ya watumishi wake.
“Kila gari la
halmashari linalopita katika daraja hili linatozwa fedha. Hasa ikizingatiwa
kuwa halmashauri hii ni mpya, hivyo watumishi wengi wanatokea nje ya
halmashauri, hiyo kwa kweli ni changamoto kubwa kwetu,”alisema Mgandilwa.
Mkurugenzi Mkuu
wa NSSF, Profesa Godius Kahyrara alikiri kupokea malalamiko ya watu wengi ambao
wanataka tozo hiyo iangaliwe upya au kuondolewa kabisa.
“Ni kweli
tumekuwa tukipokea malalamiko hayo kutoka kwa wananchi mbalimbali, lakini suala
ni kwamba sisi NSSF hatupangi viwango vya tozo za kuvuka daraja bali tunapokea
maelekezo kutoka wizara husika (Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi),” alisema Profesa
Kahyaraa.
Hata hivyo
Mkurugenzi huyo alisema atawasilisha suala hilo katika wizara husika ili kuona
uwezekano wa kuondoa tozo hiyo ama kupunguza.
Profesa
Kahyarara, alitaja changamoto zingine alizoziona tangu kufunguliwa kwa daraja
hilo kuwa ni vijana kuligeuza kuwa kijiwe na wengine kuwa na nia ovu ya
kulihujumu kwa kuharibu miundombinu, ingawa ulinzi umeendelea kuimarishwa.
Akizungumzia
suala hilo, Makonda alisema suala la tozo ya magari ya halmashauri nam
watumishi kuvuka katika daraja hilo atazungumza na waziri mwenye dhamana.
Akihutubia
wananchi wanaoishi jirani na daraja hilo, Makonda alisema tayari mkandarasi wa
ujenzi wa kipande cha barabara cha kilometa 1.5 inayounganisha daraja la
Nyerere atanza kujenga kipande hicho kwa kiwango cha lami.
“Mkandarasi
aliyejenga daraja hili ndiyo ataendelea na ujenzi wa kipande hiki
kilichobakia.Pesa zipo na ndani ya wiki mbili kuanzia sasa ujenzi
utaanza,”alisema.
Katika hatua
nyingine, mkuu huyo wa wilaya alitaja changamoto nyingine zinazoikabili wilaya
hiyo kuwa ni kipande cha Kilometa 1.5 cha barabara ya vumbi kutoka katika
daraja hilo kuelekea upande wa Kigamboni.
“Hii barabara
licha ya kutumiwa na magari mengi, haijajengwa kwa kiwango cha lami, jambo hilo
linawapa kero kubwa wananchi kutokana na kusafiri umbali mrefu katika barabara
ya vumbi,” alisema Mgandilwa.
0 comments:
Post a Comment