Joseph Sabinus
Janeth Mbene |
MBUNGE wa Ileje, Janet Mbene (CCM) ameahidi kuhakikisha changamoto
kuu za jimbo hilo za elimu, afya na barabara zinapata ufumbuzi wa kudumu.
Mbene alisema hayo hivi karibuni wakati akipokea msaada
wa vitabu vya Sayansi na Hisabati vyenye thamani ya takribani Sh milioni tano kutoka
ubalozi wa China nchini kwa ajili ya sekondari za jimbo hilo.
Katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye ubalozi huo Dar es
Salaam, Mbunge huyo alisema upungufu wa vitabu katika shule jimboni mwake, ni moja
ya changamoto zinazotokana na maendeleo katika sekta ya elimu.
“Maendeleo mengine husababisha changamoto, mfano tangu
Serikali ianze kutoa elimu bure hadi sekondari, kumekuwa na mwamko mkubwa wa
wanafunzi.
“Changamoto zilizojitokeza kwa mafanikio hayo, ni uhaba
wa vitabu, vifaa vya kufundishia, miundombinu ya vyumba vya madarasa na ukosefu
wa mabweni hasa ya wasichana sekondari,” alisema Mbene.
Alisema ukosefu wa mabweni katika sekondari, ni tishio
kwa maendeleo ya elimu kwa watoto wa kike kwa kuwa unachangia utoro, mimba na
wasichana kutofanya vizuri kwenye masomo kwa kukosa muda wa kutosha kufuatilia masomo.
“Nashukuru ubalozi wa China kwa kuitikia ombi hili.
Tutahakikisha vitabu hivi vinatumika vizuri ili shule zote zinufaike maana ni
wajibu wangu kutafuta namna ya kutatua kero za wananchi wangu likiwamo suala la
elimu, barabara na huduma za afya; hayo ni mambo makubwa yanayoninyima usingizi.
“Katika Jimbo hili, hakuna sekondari yenye bweni la
wasichana. Nataka kuhakikisha hilo linaondoka na hii itasaidia kuwa moja ya
dawa dhidi ya mimba za utotoni kwa wanafunzi,” alisema.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Balozi wa China, Ofisa
Ubalozi huo, Gov Haodong alisema China inapata faraja kushirikiana na Tanzania
kutatua kero za watoto katika sekta ya elimu.
“China itaendelea kushirikiana na Tanzania kuchangia
elimu nchini maana China kuna usemi kuwa, “watoto na wanafunzi ndio maua ya Taifa”.
“Ingawa msaada huo ni mdogo, lakini kitu kidogo
kinapotolewa kwa nia njema, kinakuwa na thamani kubwa, hivyo tutaendelea
kukuunga mkono ili kusaidia watoto wetu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment