Jemah Makamba
MSHITAKIWA wa kesi ya wizi na kujeruhi
kwa kutoboa mtu macho, Salim Njwete ‘Scorpion’ amefikishwa mahakamani kusomewa
maelezo ya awali (PH) ambapo katika mashitaka
yake alikana kutoboa macho na kuiba
lakini akakiri kuwa mwalimu wa karate na kukana kuitwa Scorpion.
Alifikishwa mahakamani hapo jana saa mbili
asubuhi akiwa kwenye gari dogo la Polisi akiwa peke yake na pingu mikononi.
Mshitakiwa alifikishwa kwenye chumba cha
Mahakama ambapo kesi yake iko mbele ya Hakimu Mkazi Flora Haule ambaye alimpaMwendesha
Mashitaka, Nassoro Katuga karatasi yenye malalamiko kwa ajili ya kumsomea mshitakiwa
maelezo hayo.
Katuga alimsomea jina lake na kumwuliza
kama ni kweli anaitwa hivyo au sivyo na mshitakiwa kusema anaitwa Salim Njwete
na kukataa jina la Scorpion akisema halitambui.
Aliulizwa kama yeye ni mwalimu wa karate
na kama alipata mafunzo ya mchezo huo kati ya mwaka 1989 na 1995 Ifakara,
Morogoro akajibu kuwa ni kweli.
Katuga alimwuliza kama aliwahi kuwa mlinzi
wa baa ya Kimboka, Buguruni, akakana.
Alipoulizwa kuhusu kuhusika na wizi kwa
kutumia kisu na kumjeruhi malalamikaji tumboni, mabegani na kumtoboa macho, pia
alikana.
Aliulizwa baada ya tukio hilo alikamatwa
na kupelekwa kituo cha Polisi, Buguruni ambako alikiri kwa maandishi kuhusika,
alikana pia.
Mwendesha Mashitaka alisema kutokana na
kifungu cha sheria cha 234 sura ya 16 kuruhusu mshitakiwa kutenganishiwa mashitaka,
katika mashitaka yanayomkabili alitenganishiwa mashitaka ya wizi na ya kujeruhi,
hivyo kuwa na kesi mbili.
Upande wa Jamhuri ulimwomba Hakimu
awapangie tarehe ya karibu ili usikilizaji kesi uanze ambapo ulisema unatarajia
kuwa na mashahidi sita.
Hakimu alisema kesi hiyo itaanza
kusikilizwa Desemba 14 na mshitakiwa ataendelea kukaa mahabusu hadi siku hiyo.
Njwete alikamatwa kwa tuhuma za kumwibia
Saidi Mrisho vitu na fedha vya thamani ya Sh 476,000 na kabla na baada ya kumwibia,
alimjeruhi kwa kumchoma kisu tumboni, mabegani na kumtoboa macho, Buguruni
Sheli.
0 comments:
Post a Comment