Edith Msuya
Augustine Mrema |
MWENYEKITI wa Bodi ya Taifa ya Msamaha kwa Wafungwa
(Parole), Agustino Mrema, amemuandikia barua Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa kumuomba
aamuaru Jeshi la Magereza, liruhusu upunguzaji wa wafungwa
magerezani kwa mujibu wa sheria za nchi.
Amesema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari
kuhusu hatua ya Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Dodoma, Antonin Kilumbi (SACP),
kusitisha upunguzaji huo wa wafungwa, baada ya kupata maagizo kutoka kwa viongozi
wa juu, huku akinukuu baadhi ya aya za barua hiyo.
"Utaratibu huu wa kupunguza wafungwa magerezani,
umefanyika baada ya wewe Waziri Mkuu kuniagiza wakati ulipokabidhiwa taarifa
kutoka kwa Mkuu wa Magereza mkoani Dodoma, ulipotembelea Gereza Kuu la Isanga
Oktoba 5 mwaka huu na kuambiwa kuna wafungwa wengi katika magereza.
"Uliniagiza nifuatilie na kutatua tatizo hilo la
msongamano wa wafungwa kwenye magereza ya Mkoa wa Dodoma," alisema Mrema
akinukuu barua hiyo mbelea ya waandishi wa habari.
Mrema ambaye aliambatanisha baadhi ya risiti za malipo ya
faini za wafungwa katika barua hiyo, alisema baada ya agizo hilo la Waziri
Mkuu, alianza kutafuta wadhamini wa kulipia wafungwa walio magerezani baada ya
kushindwa kulipa faini.
Mmoja wa wafadhili hao kwa mujibu wa Mrema ni Mchungaji
Getrude Lwakatare wa Kanisa la Assembilies of God 'Mlima wa Moto', ambaye
alikubali kutoa Sh milioni 12.84.
Alisema fedha hizo zingeweza kuwatoa wafungwa 43 walio
katika magereza ya mkoa huo baada ya kushindwa kulipa faini, hivyo kupunguza
msongamano katika magereza hayo yenye uwezo wa kuhifadhi wafungwa 1,552, lakini
yamelazimika kutunza wafungwa 1,795.
"Waziri Mkuu tunaamini kwamba kitendo hicho ni
kinyume cha utawala wa sheria na ni ukiukwaji wa amri za mahakama, ambazo
zilieleza wazi kwamba endapo washitakiwa watalipa au kulipiwa faini waachiwe
huru," alisema.
Mwenyekiti huyo alisema bado hawajapatiwa sababu za
maandishi kwa nini wafungwa waliolipiwa faini wasiachiwe, isipokuwa amesoma
kwenye magazeti kwamba upunguzaji huo wa wafungwa umesitishwa.
Mrema alisema kupungua kwa wafungwa katika magereza, kunasaidia
wafungwa kuondokana na magonjwa ya mlipuko, wafungwa wanawake wanyonyeshe na wazee
na wagonjwa na kubana bajeti.
"Lengo letu si kuwatoa majambazi, majangili na wauza
dawa za kulevya na si kama watu wanavyosema kwamba sisi tunatoa
majambazi," alisema.
0 comments:
Post a Comment