Fidelis Butahe
Dk. John Magufuli |
AHADI ni deni. Ndivyo unavyoweza kusema
baada ya Rais John Magufuli kutekeleza kwa kitendo kauli yake ya kusaini Muswada
wa Sheria ya Huduma za Habari kuwa Sheria mara tu itakapotua mezani kwake.
Novemba 4 Rais alikutana na vyombo vya
habari Ikulu, Dar es Salaam katika tukio ambalo liliwahusisha wahariri na
kueleza kuwa Muswada wa sheria hiyo kama zilivyo zingine, zimefuata utaratibu
wa kupelekwa bungeni na ukipitishwa na kuwa sheria atausaini haraka.
Jana Ikulu ilitoa taarifa ikieleza kuwa
alisaini sheria hiyo juzi huku akipongeza wadau wote kwa kufanikisha kutungwa
kwake.
“Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu inapewa
kuwataarifu kuwa Rais amesaini Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 iliyopitishwa na
Bunge la 11 katika mkutano wake wa tano Dodoma,“ ilieleza taarifa ya Ikulu.
Katika taarifa hiyo, Rais Magufuli
alisema, “naamini kuwa sheria hii itasaidia kuboresha sekta ya habari kwa
manufaa ya wanataaluma wenyewe na Taifa.”
Uamuzi huo wa Rais Magufuli huenda ukawa
mwiba mchungu kwa wadau wengi wa habari ambao walianza kupinga Muswada huo
kuwasilishwa na kupitishwa na Bunge, wakitaka wapewe miezi mitatu ya kutoa
maoni yao huku wakipendekezwa uwasilishwe bungeni mwakani.
Akizungumza hivi karibuni na JAMBO LEO Katibu
Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome alisema sheria hiyo
itaanza kutumika baada ya Waziri mwenye dhamana kuitangaza katika Gazeti la
Serikali.
Alisema katika sehemu ya kwanza ya
sheria hiyo, inaeleza kuwa itaanza kutumika baada ya kutangazwa kwenye Gazeti
la Serikali, hivyo Rais akishaisaini ni lazima itangazwe kwanza ili ianze kutumika.
“Kama sheria husika imesema itatumika
pale Waziri mwenye dhamana atakapoitangaza kwenye Gazeti la Serikali, basi utafuata
utaratibu huo ila kwanza lazima iwe imesainiwa na Rais.
“Kama sheria husika haikusema, Waziri
ataitangaza kwenye Gazeti la Serikali ili ianze kutumika, maana yake inaanza
kutumika siku hiyo hiyo ambayo imesainiwa na Rais,” ilisema taarifa.
Kuhusu kanuni za sheria husika alisema haziwezi
kusababisha sheria isianze kutumika, “Waziri husika anaweza kuziandaa kwa sababu
kanuni ni suala endelevu…ila kama sheria inajitosheleza, itaanza kutumika kwa vipengee
vyake kwa jinsi ilivyosema.”
0 comments:
Post a Comment