Leonce Zimbandu
Elius Mwakalinga |
MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Majengo
Tanzania (TBA), Elius Mwakalinga, amesema ujenzi wa mji wa Dodoma utaanza rasmi baada
ya kikosikazi kilichoteuliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kurejea mpango
kabambe wa uendelezaji wa mji huo.
Kikosikazi hicho kitapitia ramani
iliyoandaliwa mwaka 1976 kwa siku 60 tangu Novemba na kufanya maboresho
kulingana na mazingira halisi ya Dodoma.
Mwakalinga alisema hayo jana alipozungumza
na gazeti hili Dar es Salaam baada ya mwandishi kutaka kujua uendelezaji wa
ujenzi wa makao makuu ya Serikali.
Alisema wataalamu hao watapitia upya
ramani hiyo ili kuainisha maeneo ya makazi, ofisi, miundombinu, burudani na hatarishi
ya tetemeko la ardhi.
“Haiwezekani ukaanza ujenzi kwa ramani
iliyoandaliwa miaka 40 iliyopita, ni imani yangu kuwa wataalamu walioteuliwa
watatumia taaluma zao kurejea mpango kabambe wa kuendeleza mji huo,” alisema.
Alisema mpango uliobuniwa na Serikali
kufanya mapitio ya ramani utaongeza umakini katika uendelezeji wa mji, ili kuepuka
maafa yatakayojitokeza ikiwa hadhari itashindwa kuchukuliwa kabla ya
utekelezaji.
Aliongeza kuwa ni wajibu wa TBA kuhakikisha
nyumba za watumishi wa umma zinajengwa katika mazingira yaliyobainishwa na
wataalamu kwa kuzingatia vigezo vya kitaaluma.
Aidha, alisema inashauriwa kujenga
nyumba zinazopunguza madhara ya tetemeko la ardhi kwa kutumia vifaa bora vya
ujenzi.
0 comments:
Post a Comment