Warioba Igombe, Morogoro
WANAFUNZI wa sekondari ya Mtoni
Moro mkoani hapa, wamefunga shule bila kufanya mitihani ya muhula huku Mkuu wa
Shule akituhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za ada.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa
ambaye hakutaka jina lake litajwe, urasimu wa Mkuu wa Shule, Mhina Mlimbo umesababisha
shule kufungwa mapema tofauti na shule zingine nchini.
Alidai kuwa shule hiyo
ilifungwa Oktoba 15 badala ya Novemba, huku wanafunzi wakiwa hawajafanya
mtihani kama ilivyo kawaida ya shule zote nchini kufanya mitihani ya muhula
kabla ya shule kufungwa.
“Kuna mambo mengi sana
hapa shule yanayokera walimu na wazazi kutokana na vitendo vinavyofanywa na
Mkuu wa Shule, kitendo kilichosababisha wanafunzi kufunga shule mapema tofauti
na shule zingine,” alisema mtoa taarifa.
Alisema mbali na
ubadhirifu uliosababisha walimu kutolipwa mishahara yao tangu Januari, shule
hiyo pia haina Bodi, Bendera ya Taifa, wala picha ya Rais.
Alisema iwapo hatua kali
hazitachukuliwa dhidi ya wahusika, wanafunzi wanaosoma shule hiyo watafeli
masomo yao pamoja na mitihani ya Taifa akidai kuwa Mkuu wa Shule anajali maslahi
yake pekee.
Hata hivyo, Mlimbo
alikanusha tuhuma hizo akisema ni za uongo na kueleza kuwa zinaenezwa na mmoja
wa walimu ambaye alifukuzwa kazi shuleni hapo baada ya kutaka kumsaidia
mwanafunzi mtihani wa Taifa.
Kuhusu kufunga shule
mapema, Mlimbo alisema shule yake ilifungwa mapema ili kupisha mitihani ya Taifa
ya kidato cha nne, ili wanafunzi waweze kufanya mitihani katika hali ya utulivu
bila bughudha.
Mkurugenzi wa Shule hiyo, Bernadeta
Masuka alikiri kupokea tuhuma hizo akiisema kwa sasa hawezi kutoa tamko lolote,
kwani afya yake si nzuri na itakapoimarika atashughulikia changamoto zote za
shule hiyo.
0 comments:
Post a Comment