Warioba Igombe, Morogoro
MTU
anayejulikana kwa jina la Msukumwe Mlawa (35) mkulima mkazi wa Sanga kata ya
Singisa, Morogoro Vijijini amechapwa viboko 10 na kunyweshwa lita tano za maji
na wafugaji.
Diwani wa Kata hiyo, Hassan Chambago amethibitisha tukio hilo akieleza kuwa mkulima huyo mbali na kupatwa na mkasa huo, pia wafugaji hao waliondoka na mbuzi wake wapatao 10 kutoka zizini nyumbani kwake.
Chambago alisema
siku ya tukio, wafugaji watatu walikwenda nyumbani kwa Mlawa ambaye
awali aliondoa ng’ombe shambani mwake ili wasilishe migomba yake na kumwuliza
kwa nini alifanya hivyo.
“Wafugaji hawa walifika nyumbani kwa Mlawa na kumtaka awaeleze kwa nini alifukuza ng’ombe shambani wakati walikuwa wanakula nyasi na si migomba na ndipo wakamsulubu,” alisema Chambago.
Baada ya tukio hilo, mke wa Mlawa alipiga mayowe kuomba msaada lakini wananchi walichelewa kufika eneo la tukio kutokana na miji kuwa mbalimbali na ndipo wafugaji hao walipochukua mbuzi wake na kuondoka nao.
Ilidaiwa kuwa wakulima katika vijiji vilivyo Morogoro Vijijini kwa sasa wapo kwenye wakati mgumu kutokana na mwingiliano wa wafugaji walio na makundi makubwa ya mifugo yanayolisha mazao shambani kwa makusudi.
Mlawa alisema alisikitishwa na kitendo alichofanyiwa mbele ya familia yake ambapo aliitaka Serikali kuwafukuza wafugaji wote katika wilaya hiyo, kwani wamekuwa wakionea wananchi kwa madai kuwa na jeuri ya kifedha.
Regina Chonjo ambaye
ni Mkuu wa Wilaya hiyo, alisema ili kumaliza changamoto ya wakulima na wafugaji
ni lazima mifugo itambuliwe kwa kuwekwa chapa na atakayekaidi atafukuzwa ili
mifugo ipungue na wananchi waishi kwa amani.
0 comments:
Post a Comment