Jemah Makamba
Shehe Mkuu Abubakar Zubeir |
MUFTI wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakar
Zubeir, ametaka Waislamu nchini kuadhimisha siku ya Maulid kwa kufanya usafi,
kupanda miti na kuchangia damu.
Alisema hayo kwenye mkutano na waandishi
wa habari katika makao makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Dar
es Salaam jana.
Mufti Zubeir alisema Maulid ya mwaka huu
yatasomwa usiku wa Desemba 11, ambapo kitaifa yatafanyika Singida, wilayani Iramba
na siku inayofuata Desemba 12 Batraza la Maulid litasomwa kuanzia saa nne
asubuhi Shelui.
Alitumia fursa hiyo kuwataka Waislamu
nnchini watumie siku hiyo kuonesha vitendo vyema na kufanya usafi kwenye mitaa
yao na kuchangia damu ili kusaidia wenye uhitaji wa damu.
Aidha, alisema ataongoza usafi kufurahia
siku hiyo ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) kwa kuwa Uislamu ni usafi.
Alisema yeye na familia yake watafanya
usafi mtaani kwake Mikocheni na kuchangia utoaji damu.
Aliwataka Waislamu kutojiingiza kwenye
makundi ya ugaidi kwani Uislamu si ugaidi, hivyo kuwasihi waachane na tabia
hizo.
Alisema walitarajia mgeni rasmi awe
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa lakini bado hawajajibiwa maombi yao, hivyo
wakishajibiwa watu watajulishwa kabla ya siku yenyewe.
Aliwataka viongozi wa Bakwata kusimamia
na kuhimiza amani ya nchi bila kuvumilia
wenye tabia za kuharibu amani na utulivu wa nchi.
0 comments:
Post a Comment