Mwandishi Wetu
WAKATI Serikali ikijitahidi kushawishi wawekezaji wa
ndani na nje kuwekeza nchini, baadhi ya watendaji wake katika idara zake mbalimbali
wanaonekana kukwamisha juhudi hizo kwa maslahi binafsi.
Uchunguzi uliofanyw na JAMBO LEO umebaini kuwapo
watendaji hao wanakwamisha juhudi hizo za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya
Rais John Magufuli, kufikia ndoto ya Tanzania kuwa ya uchumi wa kati ifikapo
mwaka 2025.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, huku wakijali maslahi
binafsi watendaji hao wamekuwa wakikwamisha juhudi hizo kwa kukataa kuidhinisha
maombi ya baadhi ya kampuni zenye nia ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali za
viwanda nchini.
“Hivi karibuni, kampuni moja ya ndani ya nchi iliandika
barua hapa Tanesco ikionesha nia ya kuingia ubia na shirika hilo la umma ili kujenga kiwanda cha kutengeneza vifaa
mbalimbali vya umeme kama transfoma, mita za umeme (luku) na nguzo hatua ambayo
ingewezesha tuache uagizaji wa malighafi hizo kutoka nje, lakini Tanesco imekalia
barua hiyo,” kilieleza chanzo chetu ndani ya Tanesco.
Aliongeza: “Nyaraka hizo za maombo niliziona, lakini katika
hali ya kusikitisha ombi la wawekezaji hao wazalendo halikujibiwa. Sijui
Tanesco wanataka nini?”
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felschesmi
Mramba alipotafutwa kuzungumzia kadhia hiyo simu yake iliita muda mrefu bila
majibu.
Msemaji ya shirika hilo, Leila Muhaji alipopigiwa simu,
hakupokea badala yake alijibu kwa kwa ujumbe mfupi akisema: “Nipo bize.”
Hayo yanatokea wakati Serikali ya Rais John Magufuli
ikisisitiza umuhimu wa kuwa na viwanda vya ndani ili kuwainua wazalishaji wa
nchini, hali inayoelezwa ni kukwamisha juhudi za Serikali kelekea uchumi wa
viwanda ambao ungetatua tatizo la ajira.
Uchunguzi wa gazeti hili umebainisha kwamba mwitikio wa baadhi
ya idara za Serikali zinazojitegemea
ikiwamo Tanesco katika kupokea wawekezaji wa ndani umekuwa wa kusuasua hali
inayosababisha wawekezaji hao kwenye sekta ya nishati kukata tamaa na kutafuta
nchi nyingine za kuwekeza.
Kwa mujibu wa vyanzo, kwa zaidi ya miongo miwili ya
uendeshaji wake, Tanesco imekuwa ikitegemea bidhaa za kuagiza kutoka nje huku
ikishindwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wizara husika na wawekezaji.
“Kumekuwa na mizengwe inayofanywa na watendaji wa Tanesco
hii kwa namna fulani inalenga kukwamisha uwekezaji huo ili waendelee kuagiza
bidhaa hizo nje,” alisema mmoja wa mawakala wa wawekezaji na kuongeza: “Licha
ya umuhimu mkubwa wa uwekezaji huo kwa hali ya kushangaza wao hawaoni na ndiyo
maana wanaukwamisha.”
Iwapo wawekezaji wangepata nafasi hiyo licha ya kusaidia
kuinua uchumi wa taifa, wangesaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.
Faida nyingine ni pamoja na kupunguza matumizi ya fedha
za kigeni zinazotumia kuagizia bidhaa na malighafi, huku ikiifanya Tanzania
kuwa kitovu cha uzalishaji Afrika Mashariki na kupunguza gharama za maisha kwa
watanzania.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, uwepo wa viwanda vikubwa
ungechochea kuongezeka kwa viwanda vidogo vya usindikaji ambavyo vingefanya
shughuli za uzalishaji bidhaa kabla ya kupelekwa kwenye viwanda vikubwa, hivyo
kurahisisha kazi na kuwepo kwa wataalam wa daraja la kati.
0 comments:
Post a Comment