Wakulima, wafugaji wauana Rufiji



 Sharifa Marira, Rufiji

HALI tete wilayani Rufiji. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya kuibuka mgogoro kati wa wakulima na wafugaji na kusababisha vifo vya watu wawili, mkulima na mfugaji.

Vifo hivyo vimetokea baada ya wafugaji kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima, jambo lililosababisha uhasama na kuwindana.

Katika mapigano hayo mkulima Mwidini Saidi (22) wa kata ya Kilimani alichinjwa na kung’olewa macho.

Saidi alifanyiwa ukatili huo baada ya baba yake, Omary Mpange kukamata mifugo ya wafugaji na walipokuwa wakimtafuta alikimbilia Polisi.

Kwa mujibu wa kaka wa marehemu, Bashiri Saidi tukio hilo lilitokea  Novemba 19 saa 10 jioni, baada ya kundi la wafugaji waliokuwa wakimtafuta Mzee Saidi kufika nyumbani kwake akidaiwa kupiga mifugo yao ilipoingia kwenye shamba lake, lakini baba huyo alikimbia.

‘’Walifika nyumbani kumtafuta baba wakitaka wamuue lakini kwa bahati nzuri alikimbilia Polisi, wakiwa wanaondoka walimwona mdogo wangu akirudi nyumbani, wakamwambia aseme baba aliko, alipokataa walimpiga kwa mapanga wakamtupa shambani,’’ alisema Bashiri.

Baada ya kifo hicho, mgogoro uliongezeka na siku ya pili mfugaji alipigwa na kuchomwa moto na wananchi kwa kulipiza kisasi.

Jeshi la Polisi la Mkoa wa Pwani liliingilia kati suala hilo kwa  kuweka kambi katika maeneo hayo na kufanya mkutano na wananchi likieleza athari za kujichukulia sheria mkononi, jambo ambalo wananchi hao walilipinga na kuondoka mkutanoni.

“Polisi mnatuchanganya, mmeshindwa kufuatilia mgogoro huu tangu awali hadi umefikia pabaya, watu tunauana ndipo mnakuja kushauri mambo ya sheria.

“Mnapaswa kutulinda, tuna hofu katika nchi yetu utadhani wakimbizi hatuwezi kusikiliza mkutano wenu,’’ alisikika mwananchi mmoja akizungumza huku wengine wakiondoka eneo la mkutano.

Mrakibu wa Polisi Pwani, Anael Mbise alieleza kuwa Jeshi hilo limejipanga kudhibiti mauaji na askari wa Kitengo cha Kutuliza Ghasia (FFU), wamefika eneo hilo ili kulinda usalama wa wananchi wakati jambo hilo likitafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Hata hivyo, baada ya Mbunge wa Jimbo hilo, Mohamed Mchengerwa (CCM) kufika katika eneo la tukio aliwaomba wananchi kubaki kumsikiliza ili watafute ufumbuzi wa mgogoro huo, akiwataka kuwa na subira, ambapo walirejea wakitaka kujua hatima ya maisha yao.

“Nawapa pole kwa matatizo yaliyowapata, hakuna anayependa kuishi kuona watu wakiuana na kuchinjana kama kuku. Suala hili tunalishughulikia, endeleeni kushikamana, sindikizaneni mnapokwenda shambani na maeneo mengine, ufumbuzi utapatikana,” alisema Mbunge huyo.

Alisema chimbuko la mgogoro huo ni mifugo inayostahili kuwa ndani ya wilaya hiyo ambayo sasa imezidi idadi.

“Mwaka 2007 iliidhinishwa mifugo 50,000 pekee ndani ya wilaya hii, lakini sasa ni zaidi ya 450,000 na hili limetokana na baadhi ya viongozi kupenda rushwa,” alisema Mchengerwa.

Aliongeza: “Walileta ng’ombe hapa ili sisi tufe? Tunataka ikae kwa mujibu wa sheria, mifugo sasa inaenda kila mahali tofauti na maeneo ambayo ilitakiwa kuwa. Sasa Bonde la Mto Rufiji liko hatarini kukauka, tunakoelekea kama hatutasimamia sheria, tutashindwa kulima wala kufanya chochote.”

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, juzi polisi wa kituo cha Mhoro walipigwa na wafugaji kwa kuwa walionekana kutetea wananchi ambao mazao yao yameliwa na mifugo, aliiomba Serikali iingilie kati haraka ili kunusuru maisha ya watu.

Alisema kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi wiki iliyopita kilitoa siku 30 mifugo yote iliyo wilayani humo kinyume cha sheria iondoke.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo