Wankyo Gati, Arusha
SERIKALI imeanza kurekebisha sheria ya
kuzuia na kupambana na rushwa ili kubana zaidi mafisadi na kuzuia mianya ya
ulaji rushwa.
Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Anjela
Kairuki kwenye mkutano wa kujadili masuala ya kiuchunguzi wa mali ambazo
zinapatikana kwa njia ya rushwa.
Na pia kuchunguza na kubaini mali
zilizofichwa katika nchi zingine, ulioshirikisha nchi nane za Mashariki mwa Afrika
zenye taasisi za kuzuia na kupambana na rushwa.
Alisema Serikali imeanza mchakato wa
kurekebisha sheria hiyo na inasubiri Bunge lijalo kuwasilisha bungeni Muswada
wa Marekebisho ili ujadiliwe na kupitishwa.
Alisema sheria iliyopo sasa haibani mafisadi
wala wala rushwa na wapokea rushwa,
kwani faini ambazo wanapigwa watuhumiwa hawa ni ndogo kuliko kosa alilotenda.
"Unakuta adhabu zinazotolewa haziendani
kabisa na hasara inayosababishwa na mkosaji, unakuta mkosaji anasababisha
hasara ya mabilioni ya fedha, lakini analipwa fedha kidogo tu, hivyo ndio maana
tumeona tufanyie marekebisho sheria hii ili kuwabana zaidi," alisema
Kairuki.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU), Valentino Mlowola alisema kwa kipindi hiki kumekuwa na
ongezeko la wananchi ambao wanatoa taarifa za watoa rushwa, waomba rushwa na
mafisadi hii inaonesha jinsi gani wananchi hawa wameelimika na wameelewa athari
za rushwa.
Alisema hadi mwezi jana Takukuru ilikuwa
imekusanya Sh bilioni 45, sawa na asilimia 500 za fedha zilizokuwa zimefichwa
nchi zingine na ambazo zilikutwa kwa mafisadi na kutolewa kutokana na
watuhumiwa watoa na wapokea rushwa.
"Aidha, napenda kutoa mwito kwa
wananchi kuendelea kutoa taarifa za watu ambao wamejipatia fedha haramu, wenye
mali zilizotokana na rushwa na wanapotoa taarifa wasiwe waoga, kwani kuna sheria
inayowalinda na wanapotakiwa kutoa ushahidi wasiogope kwani sharia pia
inamlinda mtoa taarifa,” alisema Mlowola.
Mkurugenzi Mtendaji wa Sekta Binafsi
Tanzania, Godfrey Simbeye alimpongeza Rais John Magufuli kwa kuanzisha Mahakama
ya Mafisadi, kwani ni jambo ambalo walikuwa wakilitamani kwa muda mrefu.
Alisema wao wako tayari kushirikiana na
Serikali kukomesha tatizo la rushwa na wanaojipatia
fedha na mali kwa njia ya rushwa.
0 comments:
Post a Comment