Suleiman Msuya
Edda Sanga |
CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania
(Tamwa) kinaungana na mashirika yanayopinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na
kutetea haki za binadamu katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili huo
kwa wanawake na watoto hasa wa kike.
Hayo yalisemwa na mkurugenzi mtendaji,
Edda Sanga, katika taarifa waliyoitoa kwenye vyombo vya habari jana jijini Dar
es Salaam.
Alisema katika maadhimisho hayo ambayo
yamebeba kauli mbiu ya “Funguka! Pinga Ukatili wa Kijinsia: Elimu Salama Kwa
Wote”, inalenga kila mzazi, mlezi, ndugu na jamaa kwa kushirikiana na serikali katika
kumlinda mtoto wa kike.
Sanga alisema Tamwa kupitia kituo chake
cha usuluhishi (CRC), kinatoa huduma ya ushauri nasaha kwa wahanga wa ukatili
wa kijinsia katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi na Newala Mkoani Mtwara.
Pia, alisema taasisi hiyo itaendelea
kutumia vyombo vya habari kutoa elimu ya uelewa kwa jamii kuhusu vitendo vya
ukatili kwa wanawake na watoto.
“Tamwa inaamini kuwa ukatili wa kijinsia
unaweza kupungua endapo wazazi, walezi, walimu, ndugu, jamaa wataona umuhimu wa
kukemea vitendo hivyo kwa kushirikiana na serikali ili kuhakikisha vyombo vya
maamuzi vinalivalia njuga suala hili,” alisema.
0 comments:
Post a Comment