Suleiman Msuya
Maalim Seif Sharif Hamad |
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema
kinachoendelea kwa sasa ndani yake ni mapambano kati yake na Polisi, Serikali
na kundi la Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba.
Madai hayo ya CUF yalitolewa jana na Mwenyekiti
wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho, Julius Mtatiro wakati akizungumza na JAMBO
LEO Dar es Salaam.
Mtatiro alisema awali walikuwa
wakipambana na kundi la Lipumba ambalo walianza kulidhibiti ila kwa sasa Polisi
na Serikali wameingia moja kwa moja bila kujificha.
Alisema mapambano hayo yalianza wakati
wa mkutano mkuu maalumu ambao ulivunjwa na kundi la Lipumba huku wahusika
wakilindwa na Jeshi hilo.
Mtatiro alisema katika kuendeleza
malengo yao walimrejesha Lipumba Ofisi Kuu ya Buguruni huku wakitambua kuwa ni
kinyume na taratibu.
“Tumekuwa katika wakati mgumu kwa sababu
tunapambana na makundi matatu; Polisi, Serikali na Lipumba na kundi lake ndiyo
maana uliona walimsindikiza ofisini na katika mikutano yake wanamlinda ila sisi
wanatufanyia fujo,” alisema.
Alisema katika kuthibitisha hilo ni
mkutano wa vijana CUF wa mkoa wa Mtwara uliopangwa kufanyika Jumamosi taratibu
zote zilifanyika ila katika mazingira ya kutatanisha ulizuiwa.
Mtatiro alisema polisi walipewa taarifa
ya kuwapo Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad, lakini siku ya mkutano polisi
hao hao walibadilika.
Alisema hali hiyo ilitokea Lindi ambako
waliwazuia kufanya mkutano wa ndani kwa kile walichodai kuwa ni maagizo kutoka
juu huku upande wa Lipumba ukiendelea na mikutano.
Aidha, alipotakiwa kueleza ni wapi
wanapata fedha za kufanya mikutano wakati chama kinagubikwa na migogoro,
alisema CUF ni chama kikubwa na kinaweza kudumu na mfumo huo kwa zaidi ya miaka
10.
Mtatiro alisema wapo wabunge, madiwani,
wanachama na wapenda mabadiliko ambao wanasaidia chama, hivyo kuzuiwa ruzuku
hakuwezi kusimamisha shughuli za chama.
“Ruzuku inaweza kuzuiwa ila si kunyimwa
kwa sababu tunaipata kwa mujibu wa sharia, hivyo sisi tutaendelea kufanya siasa
kwa njia tunazozijua,” alisema.
Akizungumzia hali hiyo Naibu Katibu Mkuu
wa Chadema, Salum Mwalimu alisema hali inayotokea CUF wameizoea ila hawatarudi
nyuma hadi haki ipatikane.
Alisema Chadema kwa kutumia wajumbe wake
wa Kamati Kuu wapo katika maeneo mbalimbali nchini kufanya mikutano, huku
akikataa kubainisha kuwa mikutano hiyo inahusu nini.
“Si Edward Lowassa pekee ambaye yuko
mikoani, karibu wajumbe wa Kamati Kuu wote wametawanyika na tunafanya kazi za
kichama,” alisema.
0 comments:
Post a Comment