Fidelis Butahe
MBUNGE wa Vunjo ambaye pia ni Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amelazwa katika hospitali ya Zydus, India tangu
Novemba 11 akisumbuliwa na maradhi ya mguu.
Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zilizolifikia
gazeti hili jana, zilieleza kuwa Mbatia alipelekwa nchini humo baada ya kupata
maumivu makali ya mguu, huku matibabu aliyopewa nchini yakielezwa kutompa
nafuu.
Msaidizi wa Mwenyekiti mwenza huyo wa
Ukawa, Hamis Athuman alipoulizwa kuhusu suala hilo, alikiri kulazwa kwa
kiongozi huyo na kutaka taarifa zaidi waulizwe viongozi wa chama na Bunge kwa
kuwa yeye si msemaji.
Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na
Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya alithibitisha kulazwa kwa Mbunge huyo na
kuieleza JAMBO LEO kuwa anaendelea
vizuri na atarejea nchini siku yoyote kuanzia leo.
“Kwa sasa hali yake imeimarika na
anaweza kurejea nchini muda wowote,” alisema Owen muda mfupi baada ya kutaka
apewe muda ili kuuliza kiundani maendeleo ya afya ya Mbunge huyo.
Habari zaidi kutoka ndani ya chama hicho
zilieleza kuwa Mbatia aliondoka nchini Novemba 10, baada ya kufika nchini humo
alilazwa.
“Novemba 14 alifanyiwa upasuaji wa mguu,
kwa sasa anaendelea vizuri ingawa bado hajaruhusiwa kutoka hosptalini,”
zilieleza habari hizo.
Zilifafanua kuwa kwa muda mrefu kiongozi
huyo amekuwa akisumbuliwa na mguu na kupewa matibabu maeneo mbalimbali bila
mafanikio.
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Danda Juju
alisema Mwenyekiti huyo amepata nafuu baada ya kufanyiwa upasuaji na kufafanua
kuwa huenda akarejea nchini mwishoni mwa wiki hii kutokana na afya yake
kuimarika.
0 comments:
Post a Comment