Badrudin Yahaya na Charles James
Ummy Mwalimu |
BAADHI ya watumishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wametupiwa lawama kwa kushindwa kutimiza
wajibu wao kwa jamii na kukwamisha taasisi binafsi kushindwa kufungua hospitali
za kisasa nchini.
Kampuni ya Quality Health Limited ya
jijini Dar es Salaam ambayo ina mpango wa kufungua kliniki na maabara zaidi ya 4,000
nchini ni miongoni mwa taasisi binafsi zilizokwamishwa na watendaji hao wa wizara.
JAMBO LEO, limeona baadhi ya maombi ya
Quality Health Limited kwenda Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto yakiwa na mchanganuo wa namna kliniki hizo zitakavyofanya kazi kwa
ajili ya kuwahudumia Watanzania.
“Quality Health Limited imekusudia kufungua
kliniki na maabara za kisasa zaidi ya 4,000 nchi nzima ambazo zitakuwa zikitoa
huduma ya afya kwa gharama nafuu kwa kusaidiana na Serikali katika kuwapatia
huduma bora wananchi hususan wagonjwa.
“Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba
tunakutana na vikwazo vingi ambavyo vinakatisha tamaa. Tunatambua kuwa kuna
maeneo mengi tu nchini yanakabiliwa na ukosefu wa huduma ya afya, hivyo sisi
tunataka kuondoa hali hiyo kwa kusaidiana na serikali yetu,” alisema ofisa
mmoja wa kampuni hiyo.
Ofisa huyo alisema katika mchakato wa
kufungua huduma hiyo ya afya wameshatumia zaidi ya sh. milioni 90, hivyo
wanashangaa kuona wakikwamishwa kwenye hatua za mwisho.
Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
ina nia thabiti ya kuwapatia wananchi wake huduma bora ikiwemo ya afya na
kwamba hata, Waziri Ummy Mwalimu amekuwa akifanya kazi kubwa lakini wapo baadhi
ya watendaji wanarudisha maendeleo nyuma.
Alifafanua kuwa ana mpango wa kufungua
vituo vingi zaidi vya afya ambavyo vingekuwa na uhusiano wa karibu na madaktari
bingwa kutoka katika maeneo mbalimbali na kwamba hiyo ingechangia kuinua sekta
ya afya hasa kwa wananchi wa hali ya chini.
Historia ya Tanzania inaonesha zaidi ya
robo tatu ya wananchi wamezaliwa na kukulia katika maeneo ya vijijini sehemu
ambazo hazina huduma bora ya afya, hivyo endapo wawekezaji binafsi wakiruhusiwa
kuwekeza ni wazi itasaidia kuinua sekta hiyo na kutoa nafuu kwa hospitali za
serikali kuelemewa na wingi wa wagonjwa.
Alidai kuwa Halmashauri ya Wilaya ya
Temeke na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) iliwaruhusu kufungua
kliniki katika Jengo la Quality Centre jijini humo, lakini wakakutana na vikwazo
kutoka kwa maofisa wa wizara kwamba eneo hilo halitakiwi kuwa na kliniki.
Aliiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru) kuingilia kati suala hilo na kuona kama michakato yake ina
uhalali kwani kuna baadhi ya kliniki zimeanzishwa wakati hazijatimiza vigezo.
Ofisa huyo kutoka Quality Health
Limited, alisema vikwazo wanavyokutana navyo vinawakatisha tamaa na vinawanyima
fursa mamilioni ya Watanzania ambao walistahili kupata huduma bora ya afya kwa
gharama nafuu.
“Inakatisha tamaa kwa kweli hebu jaribu
kufikiria mtu unataka kufungua hospitali ambazo zitasaidia Watanzania wote,
lakini unanyimwa kibali, na kinachohuzunisha zaidi haupewi sababu za msingi
bali unapigwa danadana nyingi zisizo na msingi wowote,” alidai.
JAMBO LEO lilipomtafuta Msajili wa
Hospitali kutoka wizarani, Dk Pamela Sawa alisema hawezi kuwazungumzia
wawekezaji hao, kwani hakuna watu waliokuja ofisini kwake wakanyimwa usajili wa
kutoa huduma ya afya.
Dk Sawa alisema ili mtu aweze kupatiwa
usajili lazima kwanza asajili jina la kampuni yake kisha aende ofisini kwake,
ambapo atapatiwa vigezo ambavyo vinahitajika na kama atakuwa navyo wizara haitasita
kuwapatia usajili.
“Hakuna wawekezaji waliotaka kupatiwa
usajili wa kufungua vituo vya afya wakanyimwa na ofisi yangu, labda kama
hawakua na vigezo tunavyovihitaji, lakini kama wamekidhi niwahakikishie wizara
inatoa kibali kwa kila mtu mwenye sifa na kama wanasumbuliwa na watendaji
wengine basi waonane na mimi moja kwa moja,” alisema Dk Sawa.
Alisema wizara na ofisi yake vinafanya
kazi na watu wa aina zote bila kubagua na endapo kuna wawekezaji wenye vigezo
wanaohitaji usajili anawakaribisha ofisini kwake waweze kufanya kazi.
0 comments:
Post a Comment