Fidelis Butahe
Anthony Lusekelo |
MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi (GRC) la
Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo, ameingia matatani baada ya kudaiwa kuwatolea
lugha chafu majirani zake na kuanzisha vurugu akipinga kuitwa mlevi, jambo
lililosababisha ashikiliwe kwa saa kadhaa na Polisi baada ya kukamatwa.
Tukio hilo la aina yake ambalo Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro ameiambia JAMBO LEO kuwa
atalitolea ufafanuzi leo katika mkutano wake na wanahabari, lilitokea juzi asubuhi
baada ya Mchungaji huyo kupishana kauli na majirani hao karibu na nyumba
anamoishi iliyopo Kawe, Dar es Salaam.
Lusekelo jana alilitaka gazeti hili
kupuuza habari hizo kwa maelezo kuwa ni za uzushi na hata alipoelezwa kuwa amerekodiwa,
akionekana anatoa lugha chafu kwa majirani hao na kutishia kuwaua, alisisitiza
zipuuzwe.
“Achana nao hao ni uzushi tu huo, hao
watakaoandika shauri yao. Kila jambo ukijibu si sahihi, wao wameona hivyo na
kutafsiri hivyo shauri yao,” alisema Mchungaji Lusekelo.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo
walitumia simu zao za mkononi na kumrekodi Mchungaji huyo, wakati akiporomosha
matusi hayo, kuonekana akitoa vitisho na kugoma kuliondoa gari lake alilokuwa
ameegesha kwenye mtaa anaoishi, hali iliyosababisha magari mengine kushindwa
kupita.
Katika taarifa hizo na baadhi ya picha hizo
za video, zinamwonesha Mchungaji huyo akiombwa na watu wanaomfahamu kuacha
kutoa lugha chafu hadharani, kwa kuwa ni kiongozi wa kiroho, lakini alipinga kwa
maelezo kuwa majirani hao wanamdhihaki muda mrefu kwa kumwita mlevi.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Mchungaji
huyo aliyedaiwa kuwa alikuwa amezidiwa na kilevi:
“Tulimsihi aingie ndani mwake…vijana
wake walifungua lango na akaingia ndani na kusema ndio alikuwa anarudi tangu
alivyoondoa Jumanne wiki hii… Licha ya kumsihi asitoke tena nje, lakini
aliongozana na vijana hao hadi nje na kuendelea kutukana majirani hao huku
akinyeshewa mvua na alikuwa hajavaa viatu,” zilieleza habari hizo.
Baada ya Mchungaji huyo kuonekana kutokuwa
tayari kutulia, baadhi ya majirani walipiga simu Polisi, ambao walifika eneo
hilo na kumkamata.
Akizungumza tukio hilo, Kamanda Sirro
alisema atalitolea ufafanuzi leo. Awali gazeti hili lilizungumza na Kamanda wa
Polisi Kinondoni, Susan Kaganda aligoma kusema lolote, akitaka atafutwe Kamanda
huyo wa Kanda Maalumu.
0 comments:
Post a Comment