*Ni kutokana na kauli, uamuzi wake mikutanoni
*Wananchi
walalamikia kuzuiwa wauza samaki
Sharifa Marira na Leons Zimbandu
Paul Makonda |
SIKU chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda kutoa kauli ya kujivunia watumishi wanne kati ya 120 na kupiga marufuku
uuzaji samaki, mboga mboga na matunda mitaani, wananchi na wanasiasa wamesema
kauli za kiongozi huyo hazieleweki wakimtaka azitolee ufafanuzi.
Aidha, wamesema kauli za Makonda zimetoka wakati ambapo
Serikali haijajipanga na kwamba haieleweki amelenga nini kiutendaji.
Kauli za wananchi na wanasiasa hao akiwamo Makamu Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Waziri wa Tamisemi
zinaweza kutafsiriwa kuwa amekalia kuti kavu, kwa kuwa ndio waangalizi wa
shughuli za kila siku za mikoa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana, wananchi
hao walisema hawaelewi mvutano uliopo kati ya Makonda na watendaji wa ofisi
yake unasababishwa na nini, pia hawajui uamuzi wa kuzuia biashara hizo ndogo zinazosaidia
wananchi masikini kiuchumi utaisaidiaje jamii.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali za Mitaa (LAAC), Abdallah Chikota alisema katazo hilo limetolewa
mapema wakati Serikali haijaweka mipango mizuri kwenye mitaa.
Alisema wafanyabiashara wa mboga mboga au matunda
wanaopita mitaani hawajawahi kuwa kero au kuleta adha kiasi cha kusababisha wakatazwe
kufanya bishara hiyo na wengi wana mitaji midogo.
‘’Wafanyabiashara wanaopita mitaani, kwanza wengi wana
wateja wao tayari ambao wanawapitishia biashara hiyo, wanauza kwa maombi
maalumu, lakini pia wana mitaji midogo kama Sh 5,000 au Sh 10,000 mtu huyu
ukimtaka aende sokoni kupanga chini biashara yake kwa mtaji upi?’’ Alisema na
kuongeza:
“Katazo lilitolewa mapema mno wakati Serikali ikiwa
haijajipanga kwa hilo. Kama kuna wanaoona watu hao ni adha, basi ni wachache
wanaopita kwenye masuka makubwa kununua mahitaji yao ya ndani, lakini wengi
wanawahitaji watu hao wanaoleta biashara majumbani.’’
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema:
“Muulizeni mwenyewe, anaweza kutoa ufafanuzi zaidi kama hakueleweka vizuri.’’
Mkazi wa Mbagala Rangi Tatu, Juma Hassan alisema
malumbano yanayoendelea baina ya Mkuu wa Mkoa na viongozi wenzake, bado hawajui nini kinaendelea kati yao.
Alisema watu
wanahitaji maendeleo na si vijembe vinavyoendelea kwa kuitana mizigo, kwani hali ya ni pasua kichwa hakuna anayependa mipasho.
“Kama kweli wapo wafanyakazi mizigo, basi hatua
zichukuliwe, hakuna sababu kila wakati kuzungumza kwenye vyombo vya habari,”
alisema.
Alisema wananchi wanahitaji kusikia ahadi anazotoa zikitekelezwa
kwa wakati lakini viongozi wawajibishwe kwenye vikao.
Amanda Sijali mkazi wa Sinza, alisema Mkuu wa Mkoa anapaswa kuweka wazi hata majina ya watumishi
mizigo ili iwe rahisi kwa vyombo vingine kuchukua hatua.
Alisema kitendo cha kuwaamini watumishi wanne mkoa mzima,
maana yake wengine watajificha kwenye kivuli hicho, kwa kuwa hakuna hatua zinazochukuliwa.
“Tayari Makonda ametaja viongozi katika ofisi yake kuwa
ni mizigo, hivyo Serikali au wananchi
wanafaidika nini kwani hakuna hatua inayochukuliwa,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson
Bana alisema iwapo Makonda atatambua mipaka yake, atakuwa kiongozi mzuri
anayehitaji utendaji kazi.
Alisema kauli zake zinapaswa kuzingatia anazungumzia
wapi, walengwa ni kina nani ili kuondoa mkanganyiko ndani ya jamii, lakini hivi
sasa anasababisha maswali yasiyo na majibu.
“Makonda ni mtendaji mzuri ambaye anahitaji kuondoa dhana
ya kuongopa kusemana serikalini kuhusu utendaji,” alisema.
Diwani wa Majohe, Ukonga, Waziri Mwinevyale alisema Mkuu
wa Mkoa hawezi kuzungumzia wanasiasa kama yeye, kwa vile si wateuliwa wa Rais.
“Ni wajibu wa Makonda kuzungumzia watendaji walio kwenye
ofisi yake ambao wanaweza ‘kutumbuliwa’,
lakini kwa ngazi za kisiasa hana wajibu
huo kisheria,” alisema.
0 comments:
Post a Comment