Emeresiana Athanas
Juju Danda |
CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema
kitafanya mikutano ya hadhara na maandamano ya kichama bila kujali vitisho na
porojo zinazotolewa na watawala na Jeshi la Polisi, kwani suala hilo lipo
kisheria.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Juju Danda, wakati akitangaza rasmi kuanzisha mpango
wa kuimarisha chama kwa mikutano ya ndani, hadhara na shughuli zingine za
kisiasa na maandamano nchi nzima yanapohitajika.
Alisema mpango huo unatarajia kuanza
wakati wowote baada ya kufuata taratibu na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi
kuhusu mikutano hiyo.
"Mahitaji ya kufanya mikutano hiyo,
iko palepale na wakati wowote kuanzia sasa tutatoa taarifa kwa umma,"
alisema.
Kuhusu suala la kuzuia mikutano ya vyama
vya siasa, alisema kauli hizo hazina nguvu, kwani sheria ya kuruhusu kufanyika
mikutano hiyo ipo na haijafutwa na hivyo kauli hizo hazina nguvu kisheria.
"Naomba nitoe onyo kwa watawala na
vyombo vya Dola kuheshimu sharia, kwani hawako juu ya sheria. Pia polisi lazima
watoe ushahidi wa kutosha na taarifa za kuaminika kuzuia mikutano, kwani sababu
za kiintelijensia hazina mashiko," alisema.
Aidha, chama hicho hakitavumilia
viongozi ambao wamechaguliwa kikatiba na kuapa kulinda Katiba na badala yake kuivunja
na kuendesha utawala wa kiimla.
"Kazi inayofanyika kukataza kuendesha
vyama vya siasa inatafsirika kuwa ni unyongaji wa vyama vya upinzani,"
alisema.
Alisema ni vema mamlaka husika ilirejea
misimamo na matamko yao ya kukataza mikutano hiyo kupitia sheria ya Jeshi la Polisi
na sheria ya nchi, ili waone haja ya kuviachia vyama vya kisiasa kuendelea
kufanya mikutano hiyo kikatiba.
Alisema ni vema wanasiasa na vyombo vya
Dola kuacha mihemko ya kisiasa na ushabiki ili kudumisha amani ya Taifa.
0 comments:
Post a Comment