Mwandishi Wetu
WIZARA ya Maliasili na Utalii imesema
itatoa punguzo kwa Watanzania watakaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na
vivutio vya utalii vilivyo karibu na mji wa Iringa ambavyo ni Isimila, Kalenga
na Boma la Mkuu wa Wilaya kwa gharama nafuu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana
kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Habari na
Mawasiliano Serikalini cha Wizara hiyo, hatua hiyo ni kuelekea
maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani
mwaka huu sambamba na maadhimisho ya 'Karibu Kusini ' ambayo kitaifa yatafanyika Iringa kwenye viwanja vya Kichangani kuanzia leo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa wizara hiyo
itashirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Hifadhi za Kusini mwa Tanzania (SPANEST)
pamoja na wadau wa sekta ya utalii nchini.
"Lengo la maadhimisho hayo ni
kuweka uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa utalii na thamani yake, ikiwa ni pamoja
na kuutangaza utalii kwa kuhamasisha
jamii kutumia fursa za utalii zilizopo kuinua uchumi wa wakazi wa Ukanda wa
Kusini mwa Tanzania na Taifa kwa ujumla," ilieleza taarifa hiyo.
Ilisema maadhimisho hayo yataambatana na
kaulimbiu ya 'Utalii kwa Wote – Wote Wawezeshwe' inayodhihirisha kuwa Serikali
inatambua watu wenye mahitaji maalumu kama vile walemavu,
wazee na watoto, ikisisitiza miundombinu rafiki, gharama nafuu kutembelea
vivutio vya utalii na gharama nafuu za usafiri, ili kuhakikisha kwamba utalii
unahusisha watu wengi zaidi kunufaika nao.
Iliongeza kuwa katika maadhimisho hayo,
Wizara itakuwa na washiriki ambao ni idara pamoja na taasisi zake mbalimbali
zikiwamo za Utalii, Wanyamapori, Mambo ya Kale na Misitu na Nyuki.
Kwa upande wa taasisi
zitakazoshiriki ni Bodi ya Utalii
Tanzania (TTB), Chuo cha Taifa cha Utalii, Makumbusho ya Taifa, Hifadhi za
Taifa Tanzania (Tanapa), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mamlaka ya Usimamizi
ya Wanyamapori (TAWA), Mfuko wa Misitu Tanzania
(TaFF), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, (TFS), Taasisi ya Utafiti
wa Misitu na Wadau wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Ilifafanua kuwa wadau wa Sekta ya Utalii
kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini
watashiriki kuonesha bidhaa na huduma zao muhimu ambayo ni
Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya na Songwe.
0 comments:
Post a Comment