Dk. Mpango mgeni rasmi Siku ya Takwimu


Mary Mtuka

Dk. Philip Mpango
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango anatarajia kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika, yatakayofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja wa Takwimu Pato la Taifa (NBS), Daniel Masolwa alisema siku hiyo huadhimishwa Novemba 18 ya kila mwaka ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni 'Kuimarisha Takwimu za Kiuchumi kwa Mtangamano wa Kikanda, Mabadiliko ya Miundo na Maendeleo.’

"Lengo la kuuadhimisha siku hii ni kuongeza uelewa mpana kwa watumiaji wote wa takwimu Afrika, kuhusu umuhimu wa takwimu katika kupanga mipango ya maendeleo katika sekta zote za kijamii na kiuchumi barani Afrika," alisema Masolwa.

Alifafanua kuwa siku hiyo hutoa fursa kwa nchi kuthamini na kufuata malengo yaliyofikiwa katika mipango ya ndani na nje ya nchi.

Masolwa alisema kuna umuhimu wa kuboresha na kuimarisha takwimu za kiuchumi zenye ubora kwa utangamano wa kikanda barani Afrika, ili kusaidia kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kufanikisha malengo endelevu.

Kutokana na umuhimu huo, alisema ndio maana wanaadhimisha siku hiyo kitaifa, ili kuwaleta pamoja wadau wa takwimu na watakwimu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi, mashirika ya umma, vyuo vikuu vinavyolingana na jamii zima kwa ujumla.

Aliwaomba wananchi kushiriki maadhimisho ya siku hiyo ili kujionea takwimu zinavyotengenezwa, pamoja na kutoa ushirikiano.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo