Mashaka Kibaya, Korogwe
Wakati yakielezwa hayo, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel alking’aka akionesha kushitushwa na kauli hiyo akiagiza asakwe na polisi ili atoe maelezo kuhusu tuhuma zake.
“Huyu Mtendaji asihame, polisi mumkamate ili atoe maelezo,
ana tuhuma za mambo mengi na hatuwezi kuacha hadi tujiridhishe fedha za
wananchi haziwezi kupotea, taarifa zote zikusanywe ajibu,” alisema Mkuu wa
Wilaya.
Kabla ya uamuzi huo, wananchi walielezea wasiwasi wao juu ya uwepo wa taarifa kwamba Ofisa huyo amepewa barua ya uhamisho kwenda kituo kipya cha kazi katika kata ya Lewa ambako Mkuu wa Wilaya aliagiza kusitishwa uhamisho wake.
Hata hivyo, Seruli alipotafutwa na JAMBO LEO kuzungumzia
tuhuma hizo jana, alisema yupo njiani kuelekea kwa Mkuu wa Wilaya kumpa taarifa
halisi kuhusu madai yanayomkabili akisema hayana ukweli.
“Hakuna ukweli katika shutuma zote zinazoelekezwa kwangu,
kuhusu miti kukatwa mchakato wote ulifanyika kwa kuzingatia taratibu chini ya
kamati iliyoundwa.
“Hakuna uharibifu wa mazingira na wananchi walibainisha
miti iliyostahili kukatwa chini ya Bwana Miti wa Tarafa yangu,” alisema Seruli.
Awali katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi mjini
Mombo nje kidogo ya makao makuu ya wilaya, wananchi walimweleza Mkuu wa Wilaya
kuwa eneo lao limekumbwa na uharibifu wa mazingira huku viongozi wakisema
ukataji miti ni agizo la Rais.
Akiwasilisha kero yake mbele ya Mkuu wa Wilaya, mkazi wa mji huo, Kaluse Timotheo alidai, kwamba Ofisa Mtendaji wao, Seruli aliwaeleza kwamba ukataji miti unaoendelea mjini humo unafanywa ili kutengeneza madawati ikiwa ni utekelezwaji wa agizo kutoka juu.
Kauli hiyo ilionekana kumshitua Mkuu wa Wilaya ambaye alitaka kujua ilipotoka amri hiyo ambapo mwananchi huyo alimfafanulia kwamba ni kutoka kwa Rais, akimnukuu Seruli, kuwa ndiye aliyewa majibu hayo.
Mbali na kutolewa kero ya uharibifu wa mazingira kwenye
mkutano huo wa hadhara, pia wananchi hao walimweleza Ofisa Mtendaji huyo
kutafuna fedha za wananchi, huku akikosa stakabadhi kutokana na malipo wanayopasa
kuyatekeleza.
Wakati hayo yakijitokeza, wilaya ya Korogwe imekamilisha mchakato wa kutengeneza madawati na Mkuu wa Wilaya kupiga marufuku ukataji miti ili kudhibiti uharibifu wa mazingira na kutokomeza mtandao wa hujuma kwenye misitu.
Kero nyingine iliyowasilishwa na wananchi kwenye mkutano huo, ni malalamiko kuhusu mapato yanayohusu Mamlaka ya Mji wa Mombo ambapo mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Miraji alihoji fedha zao zinakokwenda huku wakikosa mrejesho.
Miraji alisema licha ya Mamlaka yao kukusanya fedha nyingi, lakini hawapati mrejesho kwa kutengenezewa barabara na kuboreshewa miundombinu mingine huku akishangazwa na Mamlaka hiyo kuwaza kuwa Halmashauri wakati haitendewi haki.
Kwa mujibu wa Miraji alipenda swali lake kujibiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ambaye hakuwa mkutanoni huku Diwani wa Mombo, Halima Juma akipigilia msumari akitaka Mombo iangaliwe kwa jicho la huruma.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel ambaye aliendesha mkutano huo hadi usiku alimtaka Mwenyekiti kuahirisha mkutano na kuahidi kuja wakati mwingine akitaja mwishoni mwa mwezi huu ili kuendelea kutatua kero za jamii.
0 comments:
Post a Comment