Sijawa Omary, Mtwara
Ummy Mwalimu |
SERIKALI imewataka watumishi wa sekta ya
afya wenye tabia ya kuwatolea lugha ya matusi kina mama wajawazito wanaoenda
kupata huduma ya kujifungua kuacha mara moja vinginevyo imejipanga
kuwashughulikia.
Wito huo umetolewa juzi na Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipokuwa akizungumza
na wananchi mkoani Mtwara katika Viwanja vya Mashujaa kwenye Uzinduzi wa Mradi
wa Tumaini la Mama (KFW) katika mikoa ya Mtwara na Lindi.
Wito huo umekuja, baada ya kinamama hao
kutoa malalamiko hayo mbele ya waziri Ummy kuhusu baadhi ya watumishi wa afya
kwa kinachodaiwa wamekuwa wakitoa lugha ya matusi kwa wagonjwa.
“Marufuku kutoa lugha ya matusi kwa
akina mama wanapokuja kujifungua na yoyote atakayeripotiwa kwa kutajwa jina
nasema hivi nitaimba na wewe. Kwa hiyo kina mama niwaombe ukimfahamu huyo
mtumishi anayekutolea lugha ya matusi tunaomba utupatie jina lake,” alisema
Ummy.
Katika hatua nyingine, Benki ya
Maendeleo ya Ujerumani (Kfw) kwa kushirikiana na Serikali imeandaa mkakati wa
kuwasaidia kinamama na watoto lengo likiwa kupunguza vifo wakati wa kujifungua
na vya watoto hao chini ya miaka mitato.
Taarifa zinaonesha kwamba hadi mwaka
2015, watoto 54 kati ya 1,000 hufariki dunia kabla ya kufikisha miaka mitano.
Hatua hiyo imefikiwa ikilinganishwa na
idadi ya mwaka 2005 ambapo watoto zaidi ya 112 kati ya kila watoto 1000
walifariki dunia.
Mwakilishi wa ubalozi wa Ujerumani nchini, Julia Hanninga ambao ndiyo
watekelezaji wa mradi huo alisema mradi huo katika mikoa hiyo ya Mtwara na
Lindi unatekelezwa kwa awamu ya pili.
Mradi huo hadi hivi sasa tayari
umeshatekelezwa katika maeneo matano, ikiwemo mkoa wa Mbeya, Tanga, Songwe na
mikoa hiyo ya Mtwara na Lindi.
0 comments:
Post a Comment