Waandishi Wetu
Anthony Lusekelo
|
MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi (GRC) la
Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo ametaja sababu za kukamatwa kwake na polisi, kisha
kuhojiwa kwa saa kadhaa, akihusisha tukio hilo na mpango wa kutengenezwa unaofanywa
na watu aliodai wamekuwa wakimfuatilia kwa takribani mwaka mmoja sasa.
Aidha, Lusekelo maarufu kwa jina la Mzee
wa Upako, amesema hakumtukana mtu, bali alitumia maneno matatu yaliyomo kwenye
Biblia; upumbuzu, ushenzi na ujinga kuelezea hoja zake na kisha kuyatafsiri
maneno hayo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na
JAMBO LEO Lusekelo alisema si kila linalosemwa, lazima lijibiwe na kwamba kwa
tukio hilo lililomkuta Jumanne iliyopita, kuna baadhi ya mambo yamekuzwa kuliko
uhalisia.
“Hii ni kashfa?” alihoji Lusekelo na
kuongeza: “Wale wanaofumaniwa na wake za watu kwenye nyumba za wageni wasemaje,
wanaokutwa wakizini kwenye magari au kupigana na walevi nao wasemaje? Nilikuwa
nyumbani kwangu kashfa iko wapi. Ni mambo ya kukuza haya sasa kosa langu liko
wapi? Wanasema mimi mlevi, hivi wamenikuta nakunywa pombe wapi?”
Jumanne iliyopita mchungaji huyo
alikamatwa na Polisi maeneo ya Kawe, wilayani Kinondoni, akidaiwa kufanya fujo
kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa tatu asubuhi alipochukuliwa na Polisi wa Kituo
cha Kawe.
Taarifa za Mzee wa Upako kufanya vurugu
zilisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, huku video aliyerekodiwa eneo
la tukio, ikionesha gari ikiwa imepaki barabarani huku akilumbana na watu
waliokuwa ndani ya nyumba na taarifa zaidi kueleza kuwa alikuwa amelewa
chakari.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa chanzo cha
tukio hilo ni kulipiza kisasi kwa jirani zake wanaoishi katika moja ya nyumba
zilizopo jirani na nyumba yake, ambao alidai wamekuwa wakimkebehi kuwa hafai
kuwa mchungaji kwa sababu ya ulevi.
Baada ya purukushani hizo, majirani hao
walipiga simu Polisi ambao walifika eneo hilo na kuondoka na mchungaji huyo.
Ijumaa iliyopita katika mkutano wake na
wanahabari, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema
Polisi inaendelea kufanya upelelezi dhidi ya tukio hilo.
Lakini juzi katika mahojiano na gazeti
hili, Mchungaji Lusekelo alisema kuwa watu aliotofautiana nao si majirani zake,
bali ni walinzi wa kampuni binafsi ya ulinzi aliodai kuwa kwa muda mrefu amekuwa
akikutana nao wakitoka nyumbani kwake.
“Wakati naingia nyumbani kwangu
nilikutana nao getini nikawauliza wametoka wapi? Badala ya kunijibu wakaanza
kutoa lugha za matusi. Nilifanya hivyo kwa sababu ya usalama wangu na sikuwa
nikifahamiana nao,” alisema.
Alisema baada ya kuanza kuwajibu walinzi
hao, waliondoka eneo hilo na kuingia katika moja ya nyumba zilizopo katika mtaa
anaoishi, “niliwafuata hapo getini na kuwaeleza kuwa sitoondoka mpaka Polisi
waje ili kubaini ndani ya ile nyumba kuna nini.”
Alisema baada ya Polisi kufika eneo hilo
hawakutaka kusikiliza maelezo yake badala
yake walimkamata.
“Wale sio majirani zangu…, hili jambo
unaweza kulichukulia upendavyo ila binafsi naona kama ni tukio la kupanga
kutokana na hali kama hii ya kukutana na watu nisiowafahamu kujitokeza mara kwa
mara,” alisema.
Huku akionesha kushangazwa na jinsi
habari hizo zilivyotikisa maeneo mbalimbali nchini, mchungaji Lusekelo alisema,
“wakati mwingine unaweza kujiona mtu wa kawaida kumbe…, kwa kweli habari zile (kuhusu
tukio hilo) ziliniogopesha sana, nadhani hata askari aliyenikamata anajuta kwa
kutotaka kunisikiliza.”
“Wakati mwingine Mungu ana mambo yake,
mambo yake yana siri nyingi. Kujibu sio busara sana,” alisema.
Mahubiri
ya jana
Akiwahubiria mamia ya waumini wake jana, Lusekelo alisema
maneno upumbavu, ushenzi na ujinga siyo matusi,
bali ni maelezo kutoka ndani ya Biblia.
Akitafsiri maneno kwa mujibu wa kitabu
hicho Lusekelo alisema neno mpumbavu maana yake ni mtu asiyefundishika kama
wale wanawali sita ambao taa zao zilizimika kabla ya kuwasili kwa bwana harusi.
Kuhusu neno mshenzi, alisema maana yake
ni mpagani asiye na hofu ya Mungu na mjinga ni mtu mwenye dhambi ya mauti anayestahili
kutupwa jehanamu.
“Hayo ni maneno ambayo napenda kuyatumia
kwa vile yapo kwenye Biblia na hata Yesu aliwahi kuyatumia, lakini nafahamu
siyo vizuri kutoa lugha ya matusi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment