Fidelis Butahe
Rais John Magufuli |
HATUA ya Rais John Magufuli kupangua
baadhi ya safu za viongozi aliowakuta na aliowateua katika kipindi kifupi tangu
aingie madarakani imewaibua wasomi ambao wametaja kuwa imetokana na mambo
makubwa matano ambayo wameyataja.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti na
JAMBO LEO wasomi hao walisema kiongozi mkuu huyo wa nchi hufanya mabadiliko
anapoona wateandaji hao wanakwamisha malengo yake ili kuifikia dira na mipango
aliyokusudia kuitekeleza katika kipindi chake cha uongozi.
Kauli za wasomi hao zimekuja wakati jana
asubuhi Rais alimtumbua Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania,
Bernard Mchomvu na kuivunja bodi hiyo kabla ya siku hiyo hiyo mchana kumteua Charles Kichere kuwa Naibu
Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, nafasi iliyokuwa wazi kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Tangu alipoapishwa Novemba 5 mwaka jana,
Rais Magufuli amekuwa akitengua uteuzi wa nafasi mbalimbali na kuteua watendaji
wengine, huku ikielezwa kuwa walioondolewa watapangiwa kazi nyingine.
Hata hivyo, wapo waliopangiwa kazi hizo
na wengine kuendelea kusota wakisubiri majukumu mapya, jambo ambalo wasomi hao
wamelielezea kuwa na maana kubwa kiutendaji.
Waliyataja mambo hayo matano kuwa ni;
uwajibikaji, uzoefu, kasi ya utendaji, kuondoa mazoea kazini na kusaka watu
sahihi katika nafasi mbalimbali.
“Hebu tazama pale TRA, hawana jipya
mwaka hadi mwaka mambo ni yaleyale ina maana bodi haitoi uongozi na haina dira.
Hilo siyo jambo jema kama unataka kuleta maboresho. Unakuwa mwenyekiti wa bodi miaka
mitatu hakuna jipya unataka miaka
mingine mitatu? Yaani ukae miaka sita bila jipya. Rais anataka viongozi
watendaji sio bora watendaji,” alisema Dk Benson Bana, mhadhiri wa Chuo Kikuu
Dar es Salaam (UDSM).
“…Rais anapofanya uteuzi kuna vigezo
vingi anazingatia, kwanza uwezo wa mtu pamoja na uzoefu. Hawa wastaafu
anaowateua kuwa wenyeviti wa bodi ni watu ambao wana uzoefu, wanaweza kusaidia
menejimenti kusonga mbele.”
Alisema uteuzi wa Rais utakuwa na shaka
iwapo anayeteuliwa ana historia mbaya ya utumishi.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha
Kilimo Sokoine (Sua), Profesa Damian Gabagambi alisema: “Kuongoza ni sawa na
kuendesha gari. Huwezi kukariri kwamba kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro
utaendesha kwa kasi gani na utakataje kona, inategemea hali ya barabara.”
Alisema Rais kazi yake ni kutazama wapi
pamelegea ili apaimarishe huku akisisitiza kuwa mtu anayeshindwa kufanya kazi
sehemu moja anaweza kufanya vizuri sehemu nyingine.
“Si jambo zuri kuwaacha watu kukaa sehemu
moja muda mrefu hata kama wameshindwa…, inasaidia sana kuongeza ufanisi, unajua
Rais amefanya kazi na watu wengi na pia ana vyanzo vingi vya kumpa taarifa juu
ya watu wote. Anapomhamisha mtu na kumpangia sehemu nyingine anakuwa na taarifa
rasmi, ama ampe kazi nyingine au asimpe,” alisema.
Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu
Mzumbe alisema: “Ni sahihi kabisa maana ilifikia mahali mpaka bodi zikawa
zinakwenda kufanya vikao nje ya nchi. Utumbuaji huu umewazindua wengi na sasa
wanaona kuwa hali imebadilika, kwamba utabaki kama ukifanya kazi, ukishindwa
utaondolewa.”
Alisema jambo hilo limerejesha nidhamu
katika utendaji wa watumishi wa Serikali na kuongeza tija kwa kiasi kikubwa.
Kuhusu uteuzi kutenguliwa na baadaye
wahusika kuteuliwa kushika nafasi nyingine alisema: “Lazima ujue sababu za
uteuzi husika kutenguliwa…, kama ukifahamu hilo unaweza kusema Rais alikosea.”
Akitolea mfano kauli iliyowahi kutolewa
na Julius Nyerere juu ya kutengua uteuzi wa mtendaji wa Serikali na baadaye
kumteua kushika wadhifa mwingine alisema Rais huyo wa Awamu ya Kwanza alitolea
mfano wa mtu anayefagia chumba chake kwamba hazuiwi kuokota shilingi na
kuirejesha mahala pake, ikiwa atagundua kuwa ilikuwa sehemu ya uchafu uliopo
katika chumba hicho.
Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria
wa Tanganyika (TLS), Francis Stolla alisema: “Madaraka ya rais kikatiba ni
makubwa na hayana ukomo. Anaweza kumweka mtu katika madaraka na anaweza
kumwondoa. Anaweza kutengeneza taasisi na kuziunganisha au kuzivunja.”
Alisema Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin
Mkapa alipokuwa madarakani aliwahi kuwajibu wanahabari kuwa ana uwezo wa
kumwondoa mtu yeyote hata kama hana tuhuma.
“Kikwete (Jakaya-Rais wa Awamu ya Nne)
aliwahi kumwondoa Magufuli (alipokuwa waziri wa Ujenzi) na kumpeleka wizara
nyingine. Watu walilalamika ila Kikwete aliwaeleza kuwa anatambua kuwa Magufuli ni mchapakazi ila alimwondoa ili
akafanye kazi nzuri kwingine,” alisema.
Alisema kwa Katiba ilivyo sasa inampa
madaraka makubwa Rais kuteua na kuondoa mtu, kuunda taasisi na kuifuta na
kusisitiza ni juu ya jamii kuona suala hilo na kuliibua katika mchakato wa
kuandika Katiba mpya.
Chekeche
Siku nne zilizopita, Rais Magufuli
alimteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani
Athuman kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.
Uteuzi huo ulifanyika ikiwa zimepita
siku 24 tangu alipotengua uteuzi wake katika nafasi ya DCI.
Rais Magufuli miezi 10 iliyopita
alitengua uteuzi wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue lakini
takribani mwezi mmoja uliopita alimteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu
cha Diplomasia.
Uteuzi wa Sefue ulitenguliwa kwa sababu
ambazo hazikutajwa huku akiahidi kumpangia kazi nyingine huku nafasi yake
ikijazwa na Balozi John Kijazi.
Rais huyo wa Awamu ya Tano pia
aliwaondoa makamishna wa Jeshi la Polisi,
Clodwing Mtweve na Paul Chagonja na kuwateua kuwa makatibu tawala wa mikoa ya
Katavi na Mwanza.
Ilielezwa na Ikulu kuwa uteuzi wa
makamishna hao wa polisi ni sawa na ule wa Majenerali wa Jeshi la Wananci wa
Tanzania kuwa Makatibu Wakuu wa Wizara, kwa lengo la kujenga nidhamu katika
utumishi wa umma.
Pia Eliakim Maswi aliteuliwa kuwa Kaimu
Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kabla ya kuondolewa na na kurejeshwa
kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, kuelezwa kuwa mabadiliko hayo
yalifanyika kwa lengo la kumtafuta mtu mwenye utaalamu wa kuendeleza kazi
iliyofanywa na Maswi.
0 comments:
Post a Comment