Moi Dodo
BENKI ya NMB imetoa kompyuta 250 kwa Serikali zilizounganishwa
na mkongo wa Taifa, ambazo zitatumika kufundishia Tehama na masomo mengine kwa
shule za msingi na sekondari.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya kompyuta
hizo juzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa
Faustin Kamuzora alisema msaada huo utainua elimu nchini.
Profesa Kamuzora ambaye alipokea kompyuta hizo kwa niaba
ya Waziri wa Ujenzi, Mwasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mabarawa alisema
msaada huo umekuja wakati mwafaka, kwani Taifa linahitaji wataalamu wa kompyuta
ambao watasaidia kuunda programu muhimu kwa sekta ya elimu na Taifa kwa ujumla.
“Maendeleo ya teknolojia yanazidi kukua na ili kuendana nayo
ni vema tukaanza kumfundisha mtoto elimu ya kompyuta akiwa mdogo au kwenye
ngazi za chini.
“Hivyo msaada wenu NMB utaharakisha ufundishaji wa Tehama
katika shule za msingi na sekondari. Vijana wanatakiwa wafundishwe mapema elimu
hiyo ili wapate kuunda programu mahususi kwa Taifa.
“Kila taifa linajivunia wataalamu wake, hivyo msaada huu
naamini utakuwa chachu ya upatikanaji wa wataalamu hao,” alisema Profesa
Kamuzora.
Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker alisema
benki hiyo imetoa msaada huo ikiamini utakuwa mwanzo wa maendeleo ya elimu ya
kompyuta nchini kwa wanafunzi wa msingi na sekondari.
0 comments:
Post a Comment