Salha Mohamed
TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya
Fahamu (MOI), imesema iko kwenye mchakato wa kutoa rufaa ya kumpeleka Baraka
Mashauri (35), kutibiwa nje ya nchi.
Kijana huyo mwenye urefu wa futi 7.4 na
matatizo ya nyonga anayetibiwa katika Taasisi hiyo, baada ya kushindwa kupata
matibabu kutokana na maumbile yake na vifaatiba vya hospitalini hapo kushindwa.
Akizungumza jana na JAMBO LEO, Dar es
Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, Jumaa Almasi alisema wako
kwenye mchakato wa kutoa rufaa.
“Anakuja kupata matibabu hapa kwetu,
tupo kwenye mchakato wa kumpa rufaa na kuipeleka wizarani ili akatibiwe nje,” alisema.
Alisema Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ndio watu wa mwisho na kufahamu ni nchi gani
wanampeleka ili aweze kupata matibabu hayo.
Awali Almasi alisema: “Ni mrefu sana
ukilinganisha na Mtanzania wa kawaida kwani ana futi 7.4, alipokuwa akitibiwa
alitakiwa kufanyiwa upasuaji wa nyonga.”
Alisema hata vitanda vinavyotumika kulaza
wagonjwa kwa ajili ya upasuaji hakimtoshi kutokana na urefu wake, huku vitanda vya
hospitalini hapo vikiwa na urefu wa futi sita tu.
Almasi alifafanua kuwa kutokana na hali
hiyo, kijana huyo anatakiwa kuagiziwa chuma maalumu kiwandani ili kitengenezwe
au akafanyiwe upasuaji huo nje ya nchi kulingana na maumbile yake.
Mashauri alipata tatizo hilo baada ya
kuanguka na kutengua nyonga ya kushoto.
0 comments:
Post a Comment